Jumatano, 4 Mei 2016

CHAMA CHA WALIMU CWT WILAYA YA RUFIJI CHAMVAMIA MKURUGENZI KIKAONI KUDAI MALIMBIKIZO YA MADAI YAO

M1Mwenyekiti wa Chama cha walimu CWT Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani Hamza Marwile akizungumza na walimu pamoja na viongozi wa halmashauri ya Rufiji katika kikao cha dhararu kilichofanyika nje ya ukumbi wa mikutano kwa lengo la kudai malimbikizo ya madai yao mbali mbali.(Picha na mpiga picha wetu)
M2Baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Rufiji wakiwa nje ya ukumbi wa mikutano wakimsubiria mkurugenzi kwa ajili ya kutoa malalamiko ya malimbikizo ya madai yao ya muda mrefu.
…………………………………………………………………………………….
NA MWANDISHI WETU, RUFIJI    
 MKURUGENZI wa halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Rashid Salum pamona na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Hatibu Chaulembo wamelazimika  kutoka nje ya kikao cha baraza la madiwani baada ya uongozi wa chama cha walimu (CWT) wilayani humo kuvamia katika kikao hicho kwa lengo la kwenda kulalamikia madai yao  ikiwemo malimbikizo ya mishahara yao.
Walimu hao wa shule za msingi na sekondari wakiongozwa na Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Rufiji walifunga safari ya kwenda katika ofisi ya Mkurugenzi huyo lakini waliambiwa yupo kikaoni ndipo walipoamua kuandamana mpaka kwenye ukumbi huo wa mikutano na ndipo walipomwandikia ujumbe wa kutaka kuonana nae ili watoe kilio chao.
Wakizungumza kwa uchungu mara baada ya Mkurugenzi na Mwenyekiti kuamua kukubali na kuamua  kuacha kuendesha kikao na kutoka nje ya ukumbi huo wa mikutano, Mwenyekiti wa CWT Hamza Marwile  pamona na Katibu wake  Antony Mangwary  ndipo walipoamua  kutoa  malalamiko yao ya malimbikizo ya madai yao mbele ya viongozi hao wa halmashauri katika kikao cha dharura kilichofanyika chini ya mti huku mvua ikiendelea kunyesha.
Mwenyekiti wa CWT Hamza Marwile alisema kwamba wameamua kufunga safari zaidi ya kilimota 75 kwa ajili ya kwenda katika ofisi za mkurugenzi kwa ajili ya kutoa kilio chao kwa  muda mrefu kutokana na walimu  walimu wa Wilaya hiyo kunyanyasika kutokana na kutopata haki zao za msingi.
Marwile alisema katika siku za nyuma walikuwa wanapeleka malalamiko ya madai yao kwa mwajiri wao ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Rufiji  lakini cha kushangaza  madai hayo bado yalionekana kutofanyiwa utekelezaji wa haraka ndio maanda wakaamua kufunga safari ya kwenda kuonana na wahusika.
Kwa upande wao baadhi ya walimu hao  waliofunga safari kwenda kutetea haki zao  za msingi akiwemo Yasinta Karo pamoja na Abdalahamani Mtupa walikuwa na haya ya kusema kuhusina na  changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao .
Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Hatibu Chaulembo amewataka walimu hao kuvuta subira na kuwa watulivu katika kipindi hiki cha madai yao kwani suala  lao litashughulikiwa haraka iwezekanavyo ili kila mmoja aweze kupata haki yake ya msingi.
Chaulembo  alisema kwamba malalamiko hayo ya walimu yanatakiwa yaangaliwe kwa jicho la tatu kwani walimu katika Taifa hili ni watu wa muhimu sana hivyo kunahitajika kufanyike juhudi za makusudi katika kulivalia njuga suala hilo la kuwalipa madai yao mbali mbali.
“Jamani pamoja na yote mimi kiukweli  hii hali imenisikitisha sana maana  leo tupo kwenye kikao chetu cha baraza la madiwani wa Wilaya ya Rufiji, lakini hatua ambayo mmeichukua walimu jamani sio jambo jema maana kikao kinaendelea sisi tupo nje haya mambo ya muhimu ilitakiwa tuyajadili kwa kina tukiwa tumekaa ofisini maana nyinyi walimu ni watu wa muhimu sana,”alisema Chaulembo.
 Akijibu malalamiko hayo kwa walimu katika kikao cha dharura kilichofanyika chini ya mti uku mvua ikinyesha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Rashid Salumu amekiri kuwepo kwa madai hayo ya walimu na kwamba na kuahidi kuyashughulikia.
“Ni kweli kuna baadhi ya walimu hawa wanamadai yao mbali mbali lakini kitu kikubwa cha msingi napenda kusema tutashirikiana bega kwa baga na viongozi wao ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kulitafutia ufumbuzi suala hili kwa haraka ili walimu waweze kupata haki yao ya msingi,”alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba kwa sasa changamoto zote zinazowakabili walimu wa wilaya ya Rufiji atayatafutia ufumbuzi wa kudumu kwa kushirikiana na idara mbali mbali na wizara zinazohusika lengo  ikiwa ni kuhakikisha madai ya walimu  wanafanyiwa utakelezaji na wanalipwa bila uonevu wowote.
 WALIMU hao wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani kwa sasa wanadai kisi cha zaidi ya milino 500 kutoka na  madai mbali mbai ikiwemo, kupandishwa madaraja,vitambulisho vya kazi,malimbikizo ya mishahara, fedha za likizo,uhamisho, pamoja na matibabu.

0 maoni:

Chapisha Maoni