Jumatano, 11 Mei 2016

MAADHIMISHO YA MIAKA SITA YA CHAMA CHA WATANZANIA WALIOSOMEA CHINA (CAAT)


unnamed
Chama cha Watanzania Waliosoma China kwa kiingereza China Alumni Association of Tanzania (CAAT) kinapenda kukukaribisha katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 6 (2010-2016) tokea kilipozaliwa. Sherehe hiyo itafanyika katika ukumbi wa Cardinal Laurian Rugambwa Social Centre pembezoni mwa kanisa la Mtakatifu  Peter (St Peter), Oysterbay Ijumaa ya tarehe 20-May-2016 kuanzia saa 8 alasiri.
Sherehe hiyo itahudhuriwa na viongozi wakubwa kutoka serikalini na baadhi ya wageni kutoka ubalozi wa China. Pamoja na burudani mbalimbali, maadhimisho hayo yatakuwa na hotuba kutoka viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wa ubalozi wa Jamhuri ya watu wa China. Kwenye sherehe hiyo pia utafanyika uzinduzi wa tovuti (website) ya CAAT.
Baada ya chakula cha pamoja cha jioni, vilevile kutakuwa na fursa ya wafanyabiashara,  wajasiliamali na wafanyakazi waajiriwa kuonyesha bidhaa au matangazo ya bidhaa au huduma wanazotoa. Dhima kuu ya tukio hilo ni;•Utambulisho wa jumuia ya CAAT ambayo inajumuisha wataalam wa taaluma mbalimbali waliohitimu mafunzo yao katika Jamhuri ya Watu wa China•Kubaini na Kuainisha fursa zinazopatikana Tanzania na China kupitia CAAT•
Maonyesho ya bidhaa na huduma mbalimbali za biashara za wanajumuia. Wote mliopata kusoma China mnakaribishwa. Hakutakuwa na kiingilio. Unaweza kushiriki kwa kuthibitisha uwepo wako kwa kupiga simu kwa Katibu Mtendaji wa CAAT kwa kupitia 0783-992020 au 0715-200090 au email gsoreku@yahoo.com

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kushirikiana na Mamlaka nyinginezo kulinda Viwanda vya ndani.

indexNa Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.
SERIKALI kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inashauriana na Wawekezaji wa Viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua pamoja na vile vilivyofungwa ili kuviwezesha viwanda hivyo kufanya kazi.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Savelina Mwijage ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuviboresha viwanda vya kizamani ili viweze kufanya kazi vizuri kwa faida ya nchi.
Mhe. Mwijage amesema kuwa, viwanda vingi vinavyotumia teknolojia ya zamani ambavyo havifanyi kazi au kuzalisha kwa kusuasua ni vile vilivyobinafsishwa ambapo katika tathmini iliyofanywa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaonyesha kuwa kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, viwanda 24 vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 37 vimefungwa kote nchini.
Aidha, katika mkoa wa Kagera, Kiwanda cha NMC Old Rice Mill kimefungwa wakati kiwanda cha Kagera Tea Co. Ltd (MARUKU) kinafanya kazi kwa kusuasua.
“Kusuasua kwa kiwanda hiki na vingine vyote nchini kunatokana na uchakavu wa mitambo katika baadhi ya Viwanda, ushindani katika soko, kupungua kwa mtaji na kutopatikana kwa malighafi”, alisema Mhe, Mwijage.
Ameongeza kuwa, Serikali inafanya majadilaino na wawekezaji wa viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua pamoja na vile vilivyofungwa ili kuviwezesha viwanda hivyo kufanya kazi tena ambapo katika majadiliano hayo yanayoendelea, yanahimiza matumizi ya ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji viwandani.
“Tunawashauri wawekezaji walioshindwa kuendesha ipasavyo viwanda vyao kuingia ubia na wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha kwa tija ili tuongeze ajira, tuzalishe bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje na kulipa kodi”, alisema Mhe. Mwijage.
Amesisitiza kuwa, Wizara yake kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine itaendelea kulinda viwanda vya ndani kwa kuhakikisha bidhaa zote ziingiazo zinakidhi viwango na zinatozwa tozo stahiki.
“Tutahakikisha kuwa tunaboresha wepesi wa kufanya biashara kwa kuondoa tozo kero na kuhakikisha kuna umeme wa uhakika wakati wote”, alisisitiza Mhe. Mwijage.

0 maoni:

Chapisha Maoni