Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuikata Azam alama tatu pamoja na magoli matatu baada ya kukiuka kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom kwa kumchezesha mchezaji ambaye haruhusiwi kucheza.
Akizungumzia hatua hiyo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas Mapunda amesema Azam ilimchezesha beki wake Erasto Nyoni akiwa na kadi tatu za njano katika mchezo wa ligi kuu ya dhidi ya Mbeya City kitendo ambacho ni tofauti na kanuni.
Amesema kutokana na kanuni na sheria za ligi kuu, timu ambayo inafanya kitendo hicho inatakiwa kukatwa alama tatu na magoli matatu hivyo na Azam imechukuliwa hatua hiyo ambayo itakuwa ni funzo kwa vilabu vingine.
“Azam walimchezesha Erasto Nyoni katika mchezo uliochezwa Februari, 20 katika uwanja wwa Sokoine, Mbeya dhidi ya Mbeya City ni kinyume na kanuni na wanatakiwa kuadhibiwa kwa kunyanganywa alama tatu na magoli matatu,” amesema Mapunda.
Aidha Mapunda amelipa onyo benchi la ufundi la Azam kuwa makini kabla ya mchezo kwa kuangalia taarifa za wachezaji kama wanaruhusiwa kucheza au wana adhabu.
Baada ya kukatwa alama sasa Azam wameshushwa nafasi moja kutoka nafasi ya pili hadi ya tatu huku wakiwa na alama 57 na nafasi ya pili ikipanda Simba ambayo ina alama 58.