Kufuatia kuboreshwa  kwa huduma za usafiri  wa  reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Kampuni ya reli ya Congo (SNCC) ,Kampuni hizi mbili za reli zimekubaliana kwa pamoja kuwatangazia wateja na umma kwa ujumla kuwa kwa sasa  huduma hizo zimeboreshwa kwa kiwango kizuri, na hivyo kuwataka wateja wake kutumia  reli hizi  kuongeza mzigo zaidi wa kusafirisha kati ya Bandari ya Dar es Salaam  Tanzania na Jamhuri ya watu wa Congo (DRC).
Viongozi   wa reli hizi mbili walikutana Dar es Salaam siku ya tarehe 13 Juni 2016 na kufanya mkutano  wa pamoja na wateja wanaosafirisha mizigo mikubwa  waliopo Dar es Salaam  pamoja na wadau wengine, siku ya tarehe 14 Juni 2016 na kuongelea kwa undani  maswala mbalimbali yanayohusu huduma ya usafiri wa reli kati ya Tanzania, Zambia na DRC.
Kwa pamoja, TAZARA       na SNCC wamefafanua kuwa wamefanya mabadiliko makubwa katika kuboresha huduma zao hasa katika kipengele cha muda wa kusafirisha mzigo kutoka Lubumbashi na Dar es Salaam kutoka  zaidi siku 40 hadi kufikia  chini ya siku 10 hivi karibuni. TAZARA yenyewe kwa sasa inasafirisha mzigo kati ya Dar es Salaam na New Kapiri Mposhi kwa wastani wa siku  tano.
Waliongeza  kuwa, kitendo cha kupungua kwa siku za kusafirisha mizigo pia kimesaidia kuondoa kabisa tatizo lililokuwepo kubwa  la wizi wa mizigo ya wateja  njiani.
Maboresho haya  yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya  uongozi yaliyofanywa    kwa reli zote mbili ikiwa ni pamoja na hatua zilizochukuliwa na wenye hisa katika kuimarisha reli kwa kuongeza mtaji na vifaa.
Kwa pamoja , TAZARA na SNCC wameelezea  masikitiko yao makubwa kuwa pamoja na mzigo mkubwa  unaosafirishwa na ukanda wa usafirishaji wa Dar es Salaam (Dar es Salaam Transport Corridor) unaojumuisha nchi za Tanzania, Zambia na DRC  kiasi cha asilimia 2% tu ndicho kinachosafirishwa kwa njia ya reli. Hali hii haikubaliki hata kidogo na wamekubaliana kuwa na mikakati ya pamoja ya  kuhakikisha kiasi hicho kinaongezeka haraka iwezekanavyo kwa kipindi cha miezi michache ijayo.
Wadau hao  wameangalia kwa makini pia jitihada zilizokuwa zinachukuliwa za kuimarisha huduma   za reli zao lakini  wametaka  kuwepo na haja ya kupitia upya  bei ya tozo za usafirishaji wa mizigo kwa kuwa usafiri wa reli  unatakiwa uwe wa bei nafuu zaidi kuliko usafiri wa barabara.
Wadau hao  wametaka reli hizo kuboreshwa kwa kurahisisha operesheni ili kuhakikisha huduma zilizoboreshwa zinatolewa kwa wenye mizigo wa DRC, Zambia na Tanzania, pia kuhakikisha mabehewa ya mizigo yanapatikana mara yanapohitajika.
Kwa hali hii,reli  hizi  mbili wamekubaliana kwa pamoja kuunganisha nguvu zao katika kuratibu shughuli nzima  ikiwa ni pamoja na  kupanga mabehewa ya mizigo  kwa ushirikiano wa pamoja wa  reli ya TAZARA, SNCC na  kampuni ya reli ya Zambia (Zambia Railways Limited).
Wadau walioshiriki katika mkutano huo wa pamoja  walikuwa ni chama cha wafanya biashara wa Kongo waishio Dar es Salaam (Congolese Business Association),  (Zambia Cargo and Logistics Limited), (Tanzania Shipping  Agents Association), (Dar es Salaam Corridor Group Limited) na (Tanzania International Container Terminal Services).
Ujumbe wa SNCC uliongozwa na Bw. Romain Kabongo ambaye ni Mkurugenzi wa Biashara na kwa upande wa TAZARA uliongozwa na Injinia Bruno Ching’andu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ndiye aliyeongoza mkutano.
Zambia-Railways-train-ZRL-624x468Moja ya treni ya ya mizigo Nchini Zambia
locomotive-snccMoja ya treni ya migizo nchini Congo