Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Ajira na Walemavu
Mhe. Dkt Abdallah Possi akizungumza watu wenye ulemavu na wadau wa
maendeleo nchini mara baada ya uzinduzi wa kanzidata kwa ajili ya watu
wenye ulemavu nchini.
Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Ajira na Walemavu
Mhe. Dkt Abdallah Possi akifatilia uwasilishwaji wa kanzidata ya watu
wenyes ulemavu nchini iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO.
………………………………………………………………………………………………..
Na Raymond Mushumbusi – MAELEZO
Bwana Joachim Marege ni mtu mwenye ulemavu
asiyeweza kutembea. Baba huyu anakofanyia kazi inabidi apande lifti hadi
ghorofa ya kumi. Siku moja nikiwa nimeongozana naye kwenye lifti mara
ghafla umeme ukakatika. Baada ya lift kufunguliwa nikamsaidia kutoka
kwenye lift na kuendelea na safari yangu lakini kwa ndugu huyu
haikuwezekana kuendelea na safari yake kwa kupanda ngazi ilibidi asubiri
kwa muda hadi umeme utakaporudi ndo akapanda lift na kwenda ofisini
kwake. Hii ni changamoto sana kwa watu wenye ulemavu katika kupata
miundombinu rafiki ya kuwawezesha katika shughuli zao za kila siku na
ambao idadi yao inaongezeka kila kukicha.
Mnamo Aprili 11 2016 Ofisi ya Taifa ya
Takwimu wakishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu walizindua kanzi data
maalum kwa ajili ya kupata takwimu za watu wenye ulemavu nchini.
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya
Duniani, zaidi ya watu bilioni moja dunia sawa na asilimia 15 ya watu
wote duniani wanakadiriwa kuwa na aina fulani ya ulemavu. Idadi ya watu
wenye ulemavu inaongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ajali,
majanga ya asili na ya kusababishwa na binadamu, ongezeko la watu hasa
wenye umri mkubwa, magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya akili na matatizo
sugu ya kiafya.
Kuongezeka huku kwa idadi ya watu wenye
ulemavu, kunasababisha mahitaji makubwa ya huduma muhimu za kijamii.
Aidha, maisha ya watu wenye ulemavu yanakuwa magumu zaidi kutokana na
unanyanyapaa kutoka kwa jamii kwa ujumla, hali ambayo inahitaji
mabadiliko ya kimtazamo. Ni ukweli ulio wazi kwamba watu wenye ulemavu
hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania wana matatizo ya
upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya ikilinganishwa
na watu ambao hawana ulemavu.
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO), karibu asilimia 80 ya watu wenye ulemavu wanaishi katika
nchi zinazoendelea. Umaskini hupunguza uwezekano wa watu wenye ulemavu
kupata huduma za kijamii na haki nyingine za kimsingi. Kwa bahati mbaya
programu nyingi za maendeleo zimeshindwa kuzingatia mahitaji maalum ya
watu wenye ulemavu kinyume na makubaliano ya kimataifa yanayosisitiza
uzingatiaji huo kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Tumeshuhudia majengo yaliyojengwa muda mrefu
hata yanayojengwa sasa mengi hayazingatii mahitaji maalum kwa watu
wenye ulemavu. Inabidi katika ujenzi miundombinu rafiki kwa wenye
ulemevu iwekwe ili kuwapunguzia adha katika maisha watu wenye ulemavu.
Pamoja na umuhimu na uelewa uliopo bado
upatikanaji wa takwimu sahihi ni tatizo hasa katika nchi zinazoendelea
kama Tanzania. Kwenye ngazi ya kimataifa, bado kuna tofauti kuhusu nini
hasa maana ya ulemavu, suala ambalo husababisha ulinganifu wa takwimu
kuwa mgumu. Katika ngazi ya kitaifa, taarifa za watu wenye ulemavu
hazitoshelezi mahitaji ya kuweka misingi madhubuti ya kupanga na
kutekeleza programu za maendeleo zinazolenga kuboresha maisha ya watu
wenye ulemavu.
0 maoni:
Chapisha Maoni