Jumatatu, 16 Mei 2016

TIMU GANI KUUNGANA NA COASTAL UNION KUSHUKA DARAJA

Wakati Coastal Union ya Tanga ikiwa imeaga rasmi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania 2015/16, swali linabaki kwa wadau wa soka nchini kwamba ni timu gani itaungana na Wagosi wa Kaya kushuka daraja kutokana na timu tano kuwa katika hatari?
Pazia la msimu wa Ligi Kuu 2015/16 linatarajiwa kufungwa Jumapili ijayo Mei 22, mwaka huu na timu tano zinazoonekana kuwa katika hatari ya kuungana na Coastal Union yenye pointi 22 (nafasi ya 16) kushuka daraja. Kati ya timu hizo tamo, mbili ndizo zitaungana na Coastal kushuka daraja hivyo kuwa na jumla ya timu tatu.
Timu zote za Ligi Kuu tayari zimecheza mechi 29 na ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka ni African Sports ya Tanga yenye pointi 26 (nafasi ya 15); Mgambo pia ya Tanga iliyojikusanyia pointi 27 (nafasi ya 14); Kagera Sugar ya Kagera iliyovuna pointi 28 (nafasi ya 13); JKT Ruvu ya Pwani iliyopata pointi 29 (nafasi ya 12) na Toto Africans ya Mwanza yenye pointi 30 (nafasi ya 11).
Kwa hali ya mambo ilivyo, licha ya kwamba Toto inaweza kujihesabu ina nafuu ikilinganishwa na timu nyingine, ukweli unabaki kuwa kwa timu zenye pointi 27 hadi 29 zinaweza kuishusha kama Wanakishamapanda hao watapoteza mchezo wa mwisho au kupata sare huku wapinzani wao wakishinda.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Toto Africans itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha Stand United, wakati JKT Ruvu mgeni wa Simba ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wenyewe Kagera Sugar watamaliza na Mwadui FC watakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga wakati Mgambo wataalikwa Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ilihali African Sports ‘Wanakimanumanu’ wataifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Mvomero mkoani Morogoro.
Mechi nyingine ya kukunja jamvi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom zitakuwa kati ya Mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Yanga itakayokuwa mgeni wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Majimaji wakati Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara.
Mchezo mwingine wenye presha utakuwa ni kwa Tanzania Prisons yenye pointi 48 ambayo licha ya kucheza na Coastal Union ambayo imeshuka daraja kwenye Uwanja wa Mkwakwani, itakuwa inafukuziwa na Mtibwa Sugar kuwa na nafasi ya nne. Mtibwa Sugar ina pointi 47.

Maadili ni Msingi wa Uwajibikaji katika Utumishi wa Umma

 
voda
Anitha Jonas – MAELEZO
 
TANGU enzi za Azimio la Arusha, suala la maadili limekuwa likisisitizwa kama nguzo muhimu katika utoaji wa huduma kwa umma. Lengo lilikuwa ni kuhakakisha kwamba kila mtumishi wa Umma anatekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.
 
Kutofanikiwa kwa Azimio la Arusha kulitokana na baadhi ya Viongozi kujua kwamba utekelezaji wa malengo ya azimio hilo ungekwamisha nia ovu waliyokuwanayo kama Watumishi wa Umma katika kuwahudumia Wananchi. Ndio maana juhudi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kutaka azimio hilo liungwe mkono hazikuzaa matunda.
 
Pamoja na kuwepo sheria, kanuni, miongozo na mikakati ya kukuza maadili kwa watumishi wa Sekta ya Umma na watu binafsi, wananchi bado wamekuwa wakilalamika kuwepo urasimu usio wa lazima wenye lengo la kutengeneza mazingira ya rushwa na huduma zisizoridhisha. Aidha, wapo baadhi ya wafanyabishara binafsi wasiozingatia maadili na hata kufikia hatua ya kuchochea utoaji wa rushwa au kuzalisha bidhaa zisizo na viwango.
 Katika jitihada za kuhakikisha kwamba watumishi wa Umma wanakuwa waadilifu na wanafuata maadili mema, Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ilibuni mikakati ya kuwa na utaratibu mpya kwa viongozi na watumishi wa Sekta za Umma na Binafsi kusaini Ahadi ya Uadilifu (integrity pledge).
 
Ahadi ya Uadilifu ni tamko rasmi na bayana la dhamira ya kuwa na mwenendo wa kimaadili na kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa. Kwa kusaini tamko hilo, mhusika au taasisi inakuwa imejipambanua kwa Umma kuwa haitajiingiza katika masuala yasiyo ya kimaadili katika utoaji huduma na uendeshaji wa biashara.
 
Kwa mujibu wa Kamishina wa Maadili Jaji Salome Kaganda, kuna aina tatu za hati za Ahadi ya Uadilifu yaani; Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, Watumishi wa Umma na Sekta binafsi ili kila kundi liwajibike kwa namna yake.
 
Akizindua Hati za Uadilifu mwezi agosti 2015, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema, kuwepo kwa Hati hizo ni hatua kubwa  muhimu na ya kihistoria katika safari ya kuboresha na kuhuisha mifumo ya uadilifu iliyopo ili iweze kwenda sambamba na mazingira na nyakati zilizopo.
Continue reading →

0 maoni:

Chapisha Maoni