Serikali inaendelea kuimarisha
ukusanyaji wa maduhuli ili kuchangia upatikanaji wa fedha za kusaidia
kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo nchini.
Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA) imekuwa miongoni mwa taasisi za Serikali ambayo imeanza
kukusanya ada zote zitokanazo na huduma inazotoa kwa njia ya
kielekroniki kwa wadau wake kufanya malipo kwa njia ya simu au benki
kabala ya kupata huduma wanayohitaji.
Hayo yamebainishwa leo Bungeni
mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harisson Mwakyembe
alipokuwa akiwasilisha mpango wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa
mwaka wa fedha 2016/2017.
“Tayari wilaya 114 kati ya 139
zinakusanya maduhuli kwa njia ya kielekroniki na kwamba ifikapo Juni,
2016 wilaya zote Tanzania Bara zitakuwa zinatumia njia ya kielekroniki
kukusanya maduhuli” alisema Dkt. Mwakyembe.
Katika kuongeza mapato, Dkt.
Mwakyembe ameongeza kuwa upo mkakati wa kuongeza kiwango cha usajili wa
vizazi na vifo nchini, ambapo RITA imeanzisha kampeni ya usajili
inayoambatana na uboreshaji wa mfumo wa usajili kwa kuweka mfumo wa
kompyuta kila wilaya ambapo kampeni hizo zilifanyika.
Wilaya ambazo kampeni hizo
zimefanyika ni Arusha na Arumeru ambapo jumla ya watu 49,548
wamesajiliwa na kupewa vyeti vyao vya kuzaliwa.
Zoezi hilo la usajili
linaendelea katika wilaya ya Kahama na baadaye litaendelea katika wilaya
16 nchini ambazo ni Bariadi, Chato, Dodoma, Igunga, Kilombero, Kilosa,
Lushoto, Maswa, Mbinga, Misungwi, Mtwara, Muleba, Nzega, Shinyanga,
Sumbawanga na Tunduru.
Waziri Mwakyembe alibainisha
kuwa Wizara hiyo kupitia RITA imekusudia kusajili zaidi ya watu 500,000
katika maeneo hayo na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Kwa mujibu wa utafiti wa afya
uliofanyika 2010, asilimia 16 ya watoto wenye umri wa miaka mitano ndio
wenye usajili na vyeti vya kuzaliwa Tanzania Bara ikilinganishwa na
Tanzania Zanzibar ambapo usajili ulikuwa ni asilimia 79.
Ili kukabiliana na hali hiyo,
RITA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto
(UNICEF) wamebaini mradi wa kusajili watoto chini ya umri wa miaka
mitano uliofanyiwa majaribio wilaya ya Temeke mwaka 2012 na kuzinduliwa
rasmi mwaka 2014 mkoani Mbeya.
Kampeni hiyo imeonesha
mafanikio na tija kwa taifa ambapo usajili umeongezeka na kufikia
asilimia 58 ambapo awali mkoa wa Mbeya usajili ulikuwa asilimia 8.7.
Kampeni hiyo ni endelevu kwa
nchi nzima ambapo mikoa itakayoanza kufanya usajili ni Mwanza, Mara,
Shinyanga, Simiyu, Geita, Iringa, Njombe, Tabora, Kagera na Dodoma.
0 maoni:
Chapisha Maoni