Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.
Frannie Leautier, ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ambapo
ameishukuru Benki hiyo kuwa mojawapo ya mashirika ya kimataifa
yanayoisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Benki
hiyo imewekeza hapa nchini kiasi cha dola Bilioni 2 sawa na zaidi ya
shilingi Trilioni 4.4 kama ruzuku na mikopo yenye riba nafuu ili
kuendeleza sekta mbalimbali ikiwemo barabara, elimu, kilimo, nishati ya
umeme, na viwanda.
Katika
mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Mpango, ameelezea kufurahishwa kwake na Dira
ya AfDB ambayo inafanana na vipaumbele vya serikali, kupitia Mpango wa
Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano ambao umelenga kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
Dira
ya Benki hiyo imejikita katika malengo matano ambayo ni kuwekeza katika
nishati ya umeme, uzalishaji wa chakula, kuendeleza viwanda,
kuiunganisha Afrika kwa mtandao wa barabara na kuboresha maisha ya watu.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia) akiwa kwenye
majadiliano na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Dkt. Frannie Leutier (katikati) na Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo Bi.
Tonia Kandiero.
Mhe.
Dkt. Mpango, amesema kuwa uwekezaji katika sekta hizo utasaidia mpango
mkubwa wa uboreshaji wa miundombinu kama vile kujenga viwanda kwa
kuhusisha sekta ya umma na binafsi-PPP, umeme wa kutosha kuendesha
viwanda, barabara ambazo zitaunganisha nchi zote za Afrika.
“AfDB
wametusaidia sana katika ujenzi wa barabara nyingi nchini Tanzania
ikiwemo barabara ya kutoka Tanga kwenda Horohoro, ambayo imerahisisha
usafiri wa kwenda nchini Kenya. Barabara nyingine zitajengwa kutoka
mpakani Kagera kupitia Kigoma kwenda Katavi, Dodoma hadi Iringa. Hili
ni jambo kubwa” Alisema Dkt. Mpango
Dkt.
Mpango amemweleza Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika-AfDB, Dkt. Frannie Leautier juu ya mpango wa serikali wa
kuimarisha sekta ya usafirishaji ikiwemo kujenga Reli ya Kati kwa
kiwango cha Kimataifa (standard gauge) ambapo kiasi cha shilingi
Trilioni 16 kinahitajika kukamilisha mradi huo.
Ameeleza
kuwa tayari serikali imetenga kiasi cha shilingi Trilioni 1 katika
bajeti yake ya mwaka huu 2016/2017 kwaajili ya kuanza kutekeleza mradi
huo mkubwa unaohusisha njia ya reli yenye urefu wa kilometa 2,190.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akifafanua jambo mbele ya
Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie
Leutier, kulia kwa Dkt. Leutier, ni Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo Bi.
Tonia Kandiero na watendaji wa Wizara.
Ameitaja
Sekta nyingine ya kipaumbele kuwa ni kilimo kwaajili ya kuzalisha
chakula kwa wingi kwaajii ya kutosheleza matumizi ya ndani na ziada yake
kuuzwa nje ya nchi huku ikitiliwa mkazo uzalishai wa malighafi
zitakazotumika katika viwanda.
Katika
mazungumzo hayo Waziri wa Fedha na Mipango alimpongeza Dkt. Leautier,
ambaye ni raia wa Tanzania, kwa kupata nafasi ya Makamu wa Rais wa Benki
ya Maendeleo ya Afrika AfDB, kuwa ni faraja na kielelezo kizuri kwa
akina mama wa Kitanzania kuwa wanaweza.
Kwa
upande wa Makamu wa Rais wa AfDB Dkt. Frannie Leautier Dkt. Leautier,
ambaye aliambatana na Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo hapa nchini, Bi.
Tonia Kandiero, amesema kuwa AfDB imesaidia na itaendelea kusaidia
miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwemo ya barabara, elimu,
kilimo, afya, sekta ya umeme ili Tanzania iwe na umeme wa kutosha
kuendesha viwanda.
“Kwa
kufanya hayo uchumi wa nchi utaimarika, vijana watapata ajira, wananchi
watakuwa na maisha bora, chakula kitazalishwa cha kutosha na kingine
kuuzwa nje ya bara la Afrika, Viwanda vitasaidia sana kiumarisha uchumi
wa nchi kwani bila viwanda ni vigumu sana kuendelea” alisema Dkt.
Leautier
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango, akitoa ufafanuzi kuhusu
vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano kwa Makamu wa Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier (Hayupo pichani).
Ameahidi
kuwa Benki yake itaendelea kusaidia kuinua sekta ya kilimo kupitia
Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kutoa mkopo wenye masharti nafuu ili
kuwawezesha wakulima wakubwa, wa kati na wadogo kupata fursa ya mikopo
hiyo itakayosaidia uzalishaji wa mazao.
Dkt.
Leautier amesema kuwa atawasilisha kwenye bodi ya benki hiyo wazo la
Tanzania kutaka kupigwa jeki katika ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango
cha kimataifa kwa kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa si tu kwa
Tanzania, bali kwa nchi zote zinazoizunguka zikiwemo zile ambazo hazina
bahari.
“Mradi
huo ukikamilika utasaidia pia kunusuru barabara ambazo zimekuwa
zikiharibika kutokana na kupitishwa mizigo mingi mizito ambayo ingefaa
kusafirishwa kwa njia ya reli ili kuzifanya barabara hizo zidumu muda
mrefu” aliongeza
Benki
ya Maendeleo ya Afrika AfDB, kupitia mfuko wake wa Maendeleo-African
Development Fund (ADF), imeahidi kutoa kiasi cha Dola Milioni 200, sawa
na shilingi 433.6 bln, kama ruzuku na mkopo wenye masharti nafuu
kwenye Mfuko Mkuu wa Bajeti wa serikali katika kipindi cha mwaka wa
fedha 2017/2018.
Imetolewa Benny Mwaipaja, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano – Wizara ya Fedha na Mipango
Mwakilishi
mkazi wa Benki hiyo Bi. Tonia Kandiero (wa kwanza kushoto) akitoa
ufafanuzi kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango. Kutoka
kushoto kwake ni Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB )
Dkt. Frannie Leutier, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benny Mwaipaja (anayeandika).
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Mwakilishi mkazi wa Benki hiyo Bi. Tonia Kandiero.
Makamu
wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier
akisoma jambo kwenye kompyuta ndogo wakati akieleza jambo kwa Mhe.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipomtembelea na
kufanya mazungumzo naye ofisini kwake Jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Makamu wa Rais
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) Dkt. Frannie Leutier.