Alhamisi, 23 Juni 2016

WAZIRI KHEIR ATANGAZA KUANZISHWA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA ZANZIBAR

2Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheir akizungumza na waandishi wa habari juu ya kuanzishwa Mamlaka za Serikali za Mitaa Zanzibar katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Kikwajuni.
1Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri Haji Omar Kheir alipokuwa akitangaza kuanzishwa Mamlaka za Serikali za Mitaa Zanzibar.
——————————————————————————–
Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,  Serikali  za Mitaa na Idara Maalum za  SMZ  Haji Omar Kheir  ametangaza  rasmi kuanzishwa  Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwateua Madiwani  56 kwa mujibu wa sheria Namba 7 ya mwaka 2014. 
 Akitangaza Mamlaka hizo katika Ukumbi  wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Waziri Haji Omar  Kheir alisema lengo la kuanzishwa Mamlaka hizo ni kuimarisha misingi ya Utawala bora Zanzibar.
 Alisema katika Mkoa wa Mjini Magharibi  kutakuwa na Mabaraza matatu ya Manispaa  ambayo ni Baraza la Manispaa la Mjini, Baraza la Manispaa la Magharibi ‘A’ na Baraza la Manispaa la Magharibi  ‘B’.
Katika Mkoa Kaskazini Unguja kutakuwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Wakati Mkoa wa Kusini Unguja kutakuwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kati na Halmashauri ya Wilaya ya Kusini.
Alisema Pemba kutakuwa na Baraza la Mji Mkoani na Baraza la Mji  Chake chake kwa Mkoa wa Kusini na Mkoa wa Kaskazini  kutakuwa na Baraza la Mji  Wete na Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni.
Aidhaa Waziri  Kheir amefuta baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizokuwepo  awali  ambazo ni Halmashauri ya Wilaya Magharibi, Halmashauri ya Wilaya ya Wete, Halmashauri ya Wilaya ya Mkoani na Halmashasuri ya Chake chake.
Amesema hatua ya kuunda  Mabaraza  zaidi ya moja ndani ya  Mkoa  wa Mjini Magharibi ni moja ya maandalizi ya Serikali  ya kuanzisha Jiji la Zanzibar  katika siku za baadae.
Aliwataka wananchi kuendelea kupata huduma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushiriki kikamilifu katika vyombo vya maamuzi kwa lengo la kukuza ustawi wa Zanzibar.
Wakati huo huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ  ametangaza majina ya Madiwani 56 aliowateua kuungana na Madiwani waliochaguliwa na wananchi kuzitumikia Mamlaka hizo.
Kwa mujibu wa uteuzi huo madiwani 36 ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 64 na madiwani 20 ni wanaume.
Ameyaagiza Mabaraza yote kuwaapisha madiwani kuyatumika mabaraza  yao na kuandaa taratibu za uchaguzi na kufanya uchaguzi wa viongozi kwa Mabaraza ya Miji na Halmsahauri  kabla ya tarehe 20 Julai mwaka huu.

0 maoni:

Chapisha Maoni