Ni ukweli usiopingika kwamba
dunia imeingia katika maendeleo ya teknolojia yanayopelekea matumizi ya
vifaa vya kisasa na vyenye utaalamu wa hali ya juu katika kufanya
shughuli mbalimbali, ambazo hapo awali zilifanywa kwa kutumia nguvu
kubwa na idadi kubwa ya watu na kwa muda mrefu.
Maendeleo hayo ya teknolojia
yamejidhihirisha katika nyanja nyingi mojawapo ni hii ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano. Ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano
umerahisisha mawasiliano na unatoa fursa kwa jamii kwa ujumla kuwa huru
zaidi katika kutekeleza majukumu yake.
Serikali inatoa fursa kwa
wananchi kutoa hoja na kero zao popote pale walipo kwa kuanzisha tovuti
katika wizara, taasisi na ofisi zake ambazo zinawezesha wananchi kupata
tarifa muhimu na kwa urahisi kuhusu wizara, ofisi ama taasisi husika na
serikali kwa ujumla.
Katika kuzingatia maendeleo hayo
ya teknolojia ya habari na mawasiliano, mwaka 2006 Rais wa awamu ya Nne
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, aliitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakati
huo chini ya Idara ya Habari -MAELEZO kuanzisha, kuratibu na kusimamia
Tovuti ya Wananchi.
Dhamira kubwa ya kuanzishwa kwa
tovuti hii ni kutokana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya Mwaka 1977 Ibara ya 18 toleo la mwaka 2005, maagizo ya Sera
ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003; na dhana ya Serikali
inayozingatia Haki za Binadamu na Utawala Bora kama ilivyoainishwa
katika Ibara ya 19 ya Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na
Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Aidha, tovuti hii inatoa fursa
kwa wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Serikali yao, kuwawezesha
watanzania popote walipo duniani kuweza kuwasilisha hoja zao, maoni na
malalamiko serikalini kwa kutumia mtandao wa intaneti .
0 maoni:
Chapisha Maoni