Jumatano, 1 Juni 2016

TAARIFA KUTOKA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO (TASWA)

indexA;KAMATI YA TUZO
 
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imemteua Makamu Mwenyekiti wa TASWA, ambaye pia Mhadhiri Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Egbert Mkoko kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania mwaka 2015/2016.
 
Pia TASWA imeteua wajumbe tisa wa kamati hiyo. Majina yao na vyombo vyao katika mabano ni Mahmoud Zubeiry (Bin Zubeiry Sports- Online), Jane John (TBC), Baruani Muhuza (Azam Media), Limonga Justine (Redio Uhuru), Maulid Kitenge (E-FM Redio), Deogratias Rweyunga (Redio One/ITV), Shaffih Dauda (Clouds Media), Asha Muhaji (Bingwa) na Nelly Mtema (Daily News).
 
Kamati inaweza kuongeza wajumbe wengine au kupunguza kwa kadri itakavyoona inafaa. Utaratibu wa kuizindua kamati hiyo unaandaliwa na sekreterieti ya TASWA. Jukumu la kamati itakuwa ni kuandaa utaratibu wa kuwapata wanamichezo watakaowania tuzo hiyo na pia kuteua washindi kwa kila mchezo.
 
Tuzo za Wanamichezo Bora zinazotolewa kila mwaka na TASWA zimepangwa kufanyika Agosti 26, mwaka huu, Dar es Salaam zikihusisha michezo mbalimbali.
 
B; ZIARA YA MAFUNZO NAIROBI
 
TASWA kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Kenya, vimeanzisha program ya ziara ya mafunzo na kubadilishana uzoefu baina ya vyama hivyo viwili, ikiwa katika makundi tofauti ya wahariri/waandishi waandamizi na kundi lingine la waandishi wa habari chipukizi.
 
Kwa kuanzia wahariri wa habari za michezo 18 au wale wenye uzoefu katika uandishi usiopungua miaka kumi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wataenda Nairobi kwa ziara ya mafunzo kuanzia Julai 6-9 mwaka huu.
Tunaamini wakirudi wataendelea kuwa waalimu wazuri kwa wale chipukizi, ambao nao watapata fursa kama hiyo siku za usoni.
Ahsanteni,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
01/06/2016

0 maoni:

Chapisha Maoni