Posted by Esta Malibiche on Nov 4,2016 in NEWS
Na. Lilian Lundo – MAELEZO – Simiyu
Morali ya ufundishaji wa walimu wa
shule ya Msingi Igaganulwa iliyoko kata ya Dutwa, Halmashauri ya Wilaya
ya Baridi Mkoani Simiyu umeongezeka na kupelekea shule hiyo kuwa na
ufulu wa juu wa wahitimu wa darasa la Saba mwaka 2016.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Robert
Majani aliyasema hayo Wilayani Bariadi wakati wa Mahojiano na timu
inayosimamia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Wilaya hiyo kuhusu
maendeleo ya taaluma ya shule yake.
“Miaka mitatu iliyopita morali ya
ufundishaji wa walimu wa shule hii ilikuwa ya chini kutokana ushirikiano
hafifu uliokuwepo kati ya walimu wakuu wa miaka ya nyuma na walimu wa
shule hii, tatizo hilo lilipelekea walimu kuondoka kwenye vituo vya
kazi kabla ya muda wa kazi kumalizika pamoja na utoro uliokithili kwa
wanafunzi,” alifafanua Mwalimu Majani.
Aliendelea kwa kusema kuwa,
kulikuwa hakuna uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za shule baina ya
uongozi wa shule, walimu wa shule hiyo na wadau wa elimu. Vile vile
kulikuwa na upungufu wa vitendea kazi pamoja na samani za ofisini hivyo
walimu kufanya kazi katika mazingira magumu.
Tatizo hilo la walimu katika shule
hiyo lilipelekea ufaulu wa chini pamoja na utoro uliokithili kwa
wanafunzi kutokana na kutokuwepo kwa uangalizi wa walimu hivyo wanafunzi
walikuwa wakienda shule pale wanapopenda.
Katika kurudisha morali ya walimu
wa shule hiyo Mwalimu Majani kupitia vikao vya kamati ya taaluma,
walimu wakorofi walikoselewa ili kurekebisha tabia, pia kamati ya shule
iliunda sungusungu ambao walikuwa wakiwakamata na kuwarudisha shuleni
wanafunzi wanaotoroka shule.
Vile vile walimu walibadilishiwa
masomo ya kufundisha baada ya kuonekana baadhi ya walimu wa masomo ya
ufundi kutofanya vizuri katika masomo hayo hivyo wakapewa masomo ambayo
wanayamudu kufundisha.
Mapato na matumizi ya fedha ya
shule hiyo vimewekwa wazi kwa walimu wote pamoja na kushirikishwa katika
upangaji wa bajeti ya shule hiyo.
Aidha Mwalimu Majani ameanzisha
programu ya kutoa chai kwa walimu wa shule hiyo kwa kutumia posho yake
ya madaraka ambapo imesaidia kupunguza muda wa walimu kwenda kunywa chai
mjini ambako ni mbali na shule.
Mabadiliko hayo yamepelekea
kuongezeka kwa hamasa ya walimu kufundisha hivyo kupandisha ufaulu wa
wanafunzi wanaomaliza darasa la saba ambapo kwa mwaka 2016 shule hiyo
imeshika nafasi ya Sita Kiwilaya kutoka nafasi ya 28 mwaka 2015.
Mwalimu Majani alisema kuwa sababu
nyingine iliyoipelekea shule hiyo kufanya vizuri zaidi mwaka huu 2016
ni pamoja na mafunzo yanayotolewa na Serikali kupitia Mpango wa Kuinua
Ubora wa Elimu Nchini (Education Quality Improvement Programme-Tanzania)
EQUIP-T ambapo walimu wamekuwa wakipata mafunzo ya kuwajengea uwezo ili
kuwapa motisha ya kazi.
0 maoni:
Chapisha Maoni