Maisha ya kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yaya Toure kwa pamoja na wachezaji walio na umri mkubwa ambao wanakipiga pamoja Man City wanaweza kuwa na muda mchache wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo au kuondolewa haraka zaidi baada ya kutolewa kauli na Mwenyekiti wa Man City, Khaldoon Al Mubarak ambayo inaonekana kuwa na utata kuhusu wachezaji hao.
Akifanya mahojiano na kituo cha CityTV, Mubarak alisema kuwa ni muda wa klabu hiyo kuanza kuwapa nafasi vijana ili na wao waweze kuonyesha uwezo wao na lakini pia kueleza kuwa kocha mpya wa klabu hiyo, Pep Guardiola anataraji kufanya hivyo.
“Tunatakiwa kuweka ulingano wa umri, kati ya wachezaji wadogo na ambao wana uzoefu na haya yote yatafanyika kwa Pep,
“Pep ana mfumo wake anavyotaka kuongoza kikosi lakini pia ana mfumo ambao anataka utumike kucheza. Nahisi atahitaji wachezaji wa aina tofauti tofauti ambao atawajumuisha katika kikosi chake,” alisema Mubarak.