Jumapili, 5 Juni 2016

WAKULIMA NA WAFUGAJI KIJIJI CHA IDODOMA MKOANI DODOMA WAANZISHA BARAZA LA USULUHISHI


Pichani
Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Tanzania (TAYODA), Jackson Kangoye (mwenye shuka la kijani) na Mbunge wa Viti Maalumu CCM Munira Mustafa Khatibu (aliyevaa hijabu) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakulima na wafugaji wa kijiji cha Idodomaa, wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma baada ya kuanzisha baraza lao huru la usuluhishi wa migogoro yao








MMKURUGENZI wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Tanzania (TAYODA)   Jackson Kangoye na Mbunge wa Viti Maalumu, Munira Mustafa Khatib (CCM) ambao ni wakulima   wamewakutanisha wakulima na wafugaji wa kijiji cha Idodoma na kuwawezesha kuanzisha baraza lao huru la usuluhishi na mapatano litakalowasaidia kijinasua na migogoro yao kabla ya kufikishwa kwenye vyombo vingine vya serikali.

Kijiji hicho kilichopo katika ukanda wa bonde la Malololo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kinapakana na wilaya ya Kilolo kwa upande wa mkoa wa Iringa na  Kilosa mkoani Morogoro kikikadiriwa kuwa na wakulima 167 na wafugaji 143.

Wakizungumza na  wakulima na wafugaji katika kijiji hicho walisema migogoro ya wakulima na wafugaji inaweza kumalizwa kama makundi hayo yatakuwa na umoja wanaoweza kuutumia kujadili changamoto zao.

 “Tumeona tuwe na baraza letu litakalotuunganisha, tunataka wakulima na wafugaji katika kijiji hiki tujihami na migogoro mikubwa inayowakumba wenzetu na hata kusababisha vifo katika maeneo mengine nchini,” alisema Kangoye.

Kangoye alisema kuanzishwa kwa baraza hilo litakalokutana kwa mara nyingine tena baadaye mwezi huu kutawawezesha wakulima na wafugaji kufahamiana, kuheshimiana na kukuza udugu utakaosaidia kulinda mipaka yao ya kilimo na ufugaji.

“Wakulima tumekubali kuweka wigo katika mashamba yetu, na wafugaji wamekubali kutusaidia katika hilo. Lengo likiwa ni kuwakumbusha wafugaji kutoingiza au pitisha mifugo yao kwenye mashamba yetu. Na hata ikitokea hivyo iwe kwa bahati mbaya au kwa kukusudia basi tutakutana na kumaliza tofauti zetu kwa kukumbusha wajibu wa kila mmoja wetu,” alisema.

Kwa upande wake Munira Mustafa Khatib alisema; “jamii isisubiri mamlaka au viongozi wa serikali waje watatue migogoro yao, popote pale walipo, wao wenyewe wanaweza kutengeneza umoja watakaoutumia kusuluhishana na kuwekana sawa pale inapotokea kutoelewana baina yao.”

Alisema mbinu hiyo inaweza kusaidia kuondokana na uhasama baina yao ambao huchochewa hasa pale migogoro yao inapofikishwa kwenye ngazi zingine za kiserikali na kisheria.

Naye  Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Umwagiliaji wa eneo hilo, Frank Mguluka  alizungumzia chimbuko la migogoro baina yao katika kijiji hicho   na kusema kuwa ,migogoro mingi imekuwa ikisababishwa na baadhi ya wafugaji wanaotafuta malisho au kupitisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

  “Baadhi ya mifugo ya wafugaji hao inachungwa na watoto wadogo ambao wakati mwingine kwao ni ngumu kuidhibiti isingie mashambani. Tunashukuru TAYODA kwa kutukutanisha na kutengeneza umoja utakaosadia kumaliza changamoto zinazotukabili,” alisema Mguluka

Twanga  Ole Nulundu ni  Mwenyekiti wa Wafugaji Kanda ya Kusini, akishukuru kwa hatua ilifanwa na taasisi ya TAYODA alisema ni mwanzo mzuri wa kuimarisha udugu baina ya wakulima na wafugaji utakaosaidia kuyatambua maeneo ya wakulima na wafugaji  ili kuisiwe na mwagingiliano.

“Kwa kupitia baraza letu hili, sisi wenyewe tungependa kuona maslai ya wakulima na wafugaji yanaheshimiwa na kulindwa. Tunataka kugeuza migogoro hiyo historia kwa kutekeleza tuliyokubaliana,”alisema.

Kwa upande wa wananchi    Enock Ole Maduma  ni   Mfugaji na mkulima katika kijiji hicho, alisema; inawezekana wakulima na wafugaji wakaishi kwa amani kama wao wenyewe watashiriki kuyadhibiti mambo yanayowaingiza katika migogoro. Na kwa kuwa na umoja wa aina hii inawezekana kabisa kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji
.

0 maoni:

Chapisha Maoni