Jumamosi, 25 Juni 2016

RIDHIWANI AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA KITUO CHA AFYA CHALINZE NA MIONO

indexiMBUNGE wa jimbo la  Chalinze, Ridhiwani Kikwete akikabidhi gari la wagonjwa (ambulance)jana, kwa mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Chalinze,dkt  Hangai ,mbunge huyo alikabidhi  magari ya wagonjwa mawili ikiwa ni pamoja na kituo cha afya Miono.
indexMBUNGE wa jimbo la  Chalinze, Ridhiwani Kikwete akiwasha gari la wagonjwa (ambulance) mara  baada ya kulikabidhi katika kituo cha afya cha Chalinze, mbunge huyo alikabidhi  magari ya wagonjwa mawili ikiwa ni pamoja na kituo cha afya Miono.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
———————————————————————-
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze mkoani Pwani,Ridhiwani Kikwete amekabidhi magari ya kubebea wagonjwa (ambulance)katika kituo cha afya cha Chalinze na Miono yote yakiwa yamegharimu zaidi ya sh.mil 200.
Ridhiwani ametoa magari hayo kwa lengo la kupunguza adha ya usafiri kwa wagonjwa hususan wanaotakiwa kwenda kupata matibabu zaidi katika hospital ya rufaa ya Tumbi na Muhimbili.
Akikabidhi magari hayo jana ,kwa mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Chalinze, dkt Rahim Hangai, mbunge huyo alisema wakati huu sio wa longolongo bali ni wakati wa kutumikia wananchi na kutekeleza yale viongozi waliyoyaahidi ndani ya jamii.
Ridhiwani alisema hatotaka kuona gari hilo haliwatendei haki wananchi hivyo aliomba litumike kwa ajili ya wagonjwa na sio vinginevyo.
Alisema awali kituo cha afya cha Miono kilikuwa na gari la kubebea wagonjwa lakini kwasasa limeharibika hivyo kuamua kupeleka gari jingine lililokuwepo kituo cha afya cha Chalinze.
“Hadi sasa tumeshakabidhi magari ya wagonjwa katika hospitali ya wilaya iliyopo Msoga ambapo tumeikabidhi gari la wagonjwa tulilokabidhiwa na mh Rais John Magufuli ,nyingine ndio hizi mbili tulizokabidhi leo”alisema Ridhiwani.
Alieleza kuwa tatizo la ukosefu wa magari hayo lipo kwenye maeneo mengi ya jimbo hilo hivyo amejipanga kushirikiana na wadau na wafadhili mbalimbali kutatua changamoto hiyo hatua kwa hatua.
Aidha Ridhiwani alisema amepokea malalamiko juu ya kulipishwa gharama za mafuta kutoka kwa wagonjwa ambao walikuwa wakilipishwa sh.30,000 hadi 80,000 kwa wale wanaotoka Miono lakini kuanzia mwezi Julai mwaka huu hakuna mgonjwa atakaetozwagharama hizo.
Nae mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Chalinze, Saidi Zikatimu alimshukuru Ridhiwani kwa niaba ya wanaChalinze na kuahidi kushirikiana nae ili kuinua maendeleo ya jimbo hilo.
Zikatimu alisema ni jumla magari matatu ambayo yametolewa hadi sasa kutokana na juhudi za mbunge huyo iwe kwa kuomba wafadhili na jitihada zake mwenyewe.
Diwani wa kata ya Bwilingu ,Lucas Rufunga pamoja na diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi walimshukuru mbunge huyo na kumuomba asichoke kushirikiana nao kuzipatia ufumbuzi changamoto nyingine zinazowakabili kwenye sekta ya afya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Chalinze, dkt Rahim Hangai alishukuru kupokea msaada huo na kusema atahakikisha linatumika kwa matumizi lengwa.
Alielezea kuwa wanampongeza mbunge huyo kwa kujitoa kwake kuwatumikia wanaChalinze.
“Umekuwa ukionyesha kwa vitendo na sio maneno, tunaamini hukutoa kwasababu ni tajiri ama una magarii mengi bali ulitoa kwa ajili ya moyo wako wa huruma na upendo wa kusaidia “alisema dkt Hangai.
Dkt Hangai alisema wanaamini ameguswa na changamoto iliyokuwa ikiwakabili ya kupunguza tatizo la usafiri.
Hata hivyo alisema magari hayo itaboresha huduma za wagonjwa na hasa mama wajawazito na watoto katika rufaa.
Dkt Hangai alielezea kuwa licha ya kutatuliwa changamoto hiyo lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya ufunguzi wa huduma za upasuaji katika jengo kutokana na ukosefu wa vifaa ili kupunguza rufaa za wajawazito, upasuaji kwenda Tumbi.
Nyingine ni uzio wa kituo, mashine ya kufulia nguo za wagonjwa, uchakavu wa jengo la (OPD) wagonjwa wa nje, jengo la huduma ya mama na mtoto, chumba cha maiti na majeruhi.
Dkt Hangai alimuomba Ridhiwani kubeba changamoto hizo ili aweze kuzitatua.
Kuhusiana na changamoto hizo Ridhiwani alisema ameyachukua yote na kuahidi kuyafanyiakazi kadri itakavyokuwa.

0 maoni:

Chapisha Maoni