MWANASHERIA
kutoka taasisi ya HAKIARDHI jijini Dar es Salaam Mafole Baraka, akitoa
somo kuhusu sheria ya ardhi ya Tanzania kwa waandishi wa habari katika
mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa, INTERNEWS na kufanyika
Wanyama Hotel, Sinza Dar es Salaam kuanzia Juni 8 hadi 9, 2016. (Picha
na INTERNEWS).
MKURUGENZI
Mkuu wa Shirika la INTERNEWS Tanzania Wence Mushi, akifafanua jambo kwa
waandishi wa habari waliopata mafunzo juu ya rasimali za gesi, mafuta
na haki ya ardhi katika Wanyama Hotel jijini Dare es Salaam kuanzia Juni
8 hadi 9, 2016. (Picha na Salum Vuai-Maelezo, Zanzibar).
MSIMAMIZI
Mkuu wa INTERNEWS Bi. Alakok Mayombo (wa pili kushoto mstari wa mbele)
na Mkurugenzi wake Wence Mushi (kushoto kwake), wakiwa katika picha ya
pamoja na waandishi walioshiriki mafyunzo yahusuyo gesi, mafuta ba haki
ya ardhi jijini Dar es Salaam. (Picha na INTERNEWS).
…………………………………………………………………………………………………………
Na Salum Vuai, DAR ES SALAAM
MIGOGORO mingi ya ardhi
inayotokea sehemu mbalimbali nchini Tanzania, husababishwa na
kutoeleweka kwa sheria ya ardhi miongoni mwa wananchi wengi.
Mwanasheria kutoka taasisi ya
HAKIARDHI ya Dar es Salaam Mafole Baraka, amesema katika mafunzo ya
waandishi wa habari yaliyofanyika Wanyama Hotel jijini humo, kwamba watu
wengi hujikuta wakipoteza haki zao kirahisi, kwa kuwa hawaelewi
chochote kuhusu sheria hiyo.
Katika mafunzo hayo ya siku mbili
yaliyoandaliwa na shirika la kimataifa la kuwainua waandishi wa habari
(INTERNEWS), Baraka alisema migogoro hiyo imekuwa ikisababisha ugomvi
kati ya wanafamilia, wanavijiji na halmashauri za maeneo husika.
Aliyataja baadhi ya mambo
yanayoibua migogoro kuwa ni pamoja na kujitokeza kwa kadhia nyingi za
ardhi kuuzwa zaidi ya mara moja, na wakati mwengine viongozi wa familia
kuamua kuuza bila kushirikisha wenzao.
Alifahamisha kuwa kuundwa kwa taasisi ya HAKIARDHI kumelenga kusaidia kupunguza migogoro ya aina hiyo kama si kuyamaliza kabisa.
Alibainisha baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana na taasisi yake katika kupunguza migogoro hiyo kuwa na
kuweza kushawishi uundaji wa mabaraza ya ardhi ya vijiji, kusuluhisha
baadhi ya migogoro, huku kesi nyengine zikiwa zinaendelea katika
mahakama mbalimbali.
Aidha alisema hadi sasa
wamefanikiwa kuvifikia zaidi ya vijiji elfu mbili, na kwamba wananchi
wameelimika vya kutosha na kuweza kudai na kutetea haki zao mara baada
kupata elimu juu ya sheria za ardhi.
“Si hayo tu, bali pia
tumefanikiwa kushawishi watunga sera kuziimarisha sheria za ardhi
ikiwemo kutajwa kwenye rasimu ya katiba mpya,” alieleza mwanasheria
huyo.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na
changamoto kadhaa ikiwemo ya kifedha, ambayo inahitajika ili malengo ya
taasisi kuifikia nchi nzima yaweze kufanikiwa.
Baraka alisema mbali na hayo, utashi wa kisiasa nao umekuwa ukichangia sana kuendelea kwa migogoro mingi ya ardhi.
Ili kuipatia ufumbuzi migogoro
hiyo, alishauri kuendelea kutolewa elimu kwa wananchi, kuheshimu sheria
za ardhi, kupima maeneo na kuviimarisha vyombo vya utatuzi wa migogoro
hiyo.
Mapema, Mkurugenzi wa INTERNEWS
Tanzania Wence Mushi, alisema ni jukumu la waandishi wa habari kutumia
taaluma yao kuibua na kuelekeza njia ya kumaliza changamoto mbalimbali
zinazowagusa wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi.
Alisema tasnia ya habari ina
nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika nchi yoyote, hivyo ni
vyema wajikite katika kufanya uchunguzi na kuandika kadhia za aina hiyo,
pamoja na mafanikio yanayopatikana baada ya mamlaka za juu kuzinduka
kutokana na taarifa zinazoandikwa.
Katika siku ya kwanza ya mafunzo
hayo, mkufunzi kutoka taasisi ya FAWOPA (Faidika Wote Pamoja) Balthazar
Komba, alizungumzia kwa kina kuhusu miradi ya gesi nchini, changamoto
zake na matumaini ya Watanzania kushuhudia matunda ya nishati hiyo.
Akitoa shukurani kwa niaba ya
washiriki wenzake, mwandishi wa kituo cha televisheni cha Chanel Ten
David Ramadhan, alisema mafunzo waliyopata yamewapa uelewa kubwa juu ya
namna ya kuripoti masuala mbalimbali yanayogusa maslahi ya umma na
taifa.
Alisema hiyo ni hatua muhimu na
kuahidi kuwa wataongeza jitihada katika kuibua na kuandika mambo
tofauti yanayohitaji kupatiwa majibu kwa lengo ya kuinua maisha ya
Watanzania.
0 maoni:
Chapisha Maoni