Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na
Daktari Mkuu wa Hospitali ya Nanjing Dkt. Zhou Yujie akimkabidhi
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi mmoja vitabu vitakavyotumika
kuendesha mafunzo ya madaktari na wauguzi wa Zanzibar.
Dkt. Zhou Yujie ambae ni
Mkurugenzi na Daktari Mkuu wa Hospitali ya Nanjing akizungumza na
madaktari na wauguzi watakaoshiriki mafunzo ya miaka mitatu nchini China
na Zanzibar wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo uliofanyika Hospitali ya
Mnazi mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Mnazi mmoja Dkt. Ali Salum Ali akizindua mafunzo ya madaktari na
wauguzi yatakayofanyika katika Hospitali ya Nanjing na Hospitali kuu ya
Mnazi mmoja Mjini Zanzibar, (kushoto) ni Mkurugenzi wa Idara ya Elimu
na Daktari Mkuu wa Hospitali kuu ya Jimbo la Nanjing
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar
…………………………………………………………………………….
Jimbo la Nanjing Nchini China
limeongeza ushirikiano mpya na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kuanzisha mpango maalumu wa mafunzo ya miaka mitatu kwa madaktari na
wauguzi wa Hospitali kuu ya Mnazi mmoja.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kwa
zamu katika Hospitali ya Mnazi mmoja na Hospitali ya Nanjing
yatawashirikisha madaktari sita na wauguzi sita kutoka sehemu ya wazazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Mnazi mmoja Dkt. Ali Salum Ali ameyazindua rasmi mafunzo hayo na
kueleza kuwa wamejiandaa vizuri ili kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika
kwa ufanisi.
Amesema mafunzo hayo yanatarajiwa
kuwaongezea uwezo madaktari wazalendo na wauguzi katika kukabiliana
na vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua na watoto wachanga.
Dkt. Ali Salum amesema katika
mpango huo, madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Nanjing watakaoendesha
mafunzo hayo wataambatana na wanafunzi wao kwa awamu katika hospitali ya
Jimbo hilo na Hospitali ya Mnazi mmoja.
Ameongeza lengo la kuendesha
mafunzo hayo katika vituo viwili tofauti, China na Zanzibar, ni kuwapa
fursa madaktari na wauguzi kujifunza kwa kutumia mazingira ya nyumbani
na mazingira ya kigeni ambapo yatakuwa na ufanisi zaidi.
“Mara nyingi vijana wetu
wanapokwenda nje ya nchi kwa mafunzo hutumia teknolojia ya huko na
wanaporudi wanatumia teknolojia ya kwetu hivyo baadhi ya wakati
wanajikuta wapo njia panda,” aliongeza Mkurugenzi Mtendaji.
Amesisitiza kwamba mpango huo
mpya wa mafunzo utatoa fursa kwa madaktari na wauguzi wengi kutoka
Zanzibar kupata mafunzo kwa wakati mmoja na utapunguza gharama za
kuwasafirisha watu wachache kwa gharama kubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Mnazi mmoja alisema baada ya madaktari na wauguzi hao kumaliza
mafunzo yao watasaidia kutoa huduma katika Hospitali na vituo vyengine
vya afya vya Zanzibar.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu
ambae pia ni daktari mkuu wa Hospitali ya Nanjing Dkt. Zhou Yujie
amesema tayari wameandaa mtaala na kufanya uteuzi wa madaktari 20
watakaosimamia mafunzo hayo.
Katika uzinduzi wa mafunzo hayo
uliofanyika Hospitali ya Mnazi mmoja, Dkt. Zhou alimkabidhi Mkurugenzi
Mtendaji vitabu vitakavyotumika katika kuendesha mafunzo hayo.
Alisema katika mafunzo hayo
wakufunzi kutoka Hospitali ya Nanjing watashirikiana na wanafunzi wao
kuwafanyia matibabu ya kawaida na upasua wagonjwa ikiwa ni miongoni mwa
mafunzo yao.
Amekumbusha kuwa uhusiano wa
sekta ya afya kati ya Jimbo la Nanjing na Zanzibar ulianza tokea mwaka
1964 kwa kuleta madaktari katika Hospitali ya Mnazi mmoja na Hospitali
ya Abdalla Mzee Mkoani na mpango wa sasa wa mafunzo ya miaka mitatu ni
muendelezo wa historia hiyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni