Ijumaa, 10 Juni 2016

Dkt. Ali Mohamed Shein amesema yeye siyo kiongozi Dikteta

dk Na Is-haka Omar, Zanzibar.
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema yeye siyo kiongozi Dikteta kwani hajawani kumfukuza kiongozi yeyote wa kisiasa ndani ya Chama chake kwa ajili ya kulinda maslahi binafsi.
Alimtaja Katibu Mkuu wa Chama cha CUF,Maalim Seif Sharif Hamad kuwa amekuwa akizua na kuzusha uongo kwa wafasi wake kwa kuwaaminisha kwamba Dkt. Shein ni kiongozi Dikteta anayetawala Zanzibar kwa mabavu jambo ambalo sio la kweli.
Ufafanuzi huo Dkt.Shein ameutoa wakati akizungumza na Mabalozi (wajumbe wa nyumba kumi) , Wenyeviti na Makatibu wa matawi, vijana na Wazee wa CCM katika ziara zake alizofanya hivi karibu huko katika Wilaya ya Mfenesini Kichama kwenye Ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu za Mwl. Nyerere Tawi la Zanzibar Bububu.
Katika ziara hizo zlizokuwa na lengo la kuwashukru wafuasi wa Chama na wananchi kwa ujumla walioichagua CCM kwenye uchaguzi Mkuu wa Marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu pamoja na kuimarisha kuongeza kasi za kiutendaji ndani ya  Chama, Dkt. Shein aliwataka wananchi kupuuza kauli na misimamo ya wapinzani hasa Maalim Seif kwani hoja zao hazina nia ya kuwaunganisha wananchi bali ni za utengano.
Dkt. Shein alisema bango lililobebwa na Maalim Seif lililokuwa likimtangaza Rais wa Zanzibar kuwa ni Dikteta ni moja ya siasa zilizopitwa na wakati na kupingana na dhamira ya kuanzishwa kwa Mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, ulioasisiwa kwa nia ya kufanya siasa za uchumi na maendeleo kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.
“Mimi sio Dikteta kwani sijaingia madarakani kwa ubabe na mabavu kilichoniweka madarakani ni nguvu ya umma kupitia Uchaguzi wa Kidemokrasia na kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 91.
Sasa huyo anayenitangaza eti mimi ni Dikteta kweli maana ya neno hilo anayajua ama anasema kuwaridhisha wafuasi wake, akae akijua kwamba hawezi kunichafua kwa njia hiyo kwani kinga yangu ni Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 niliyoapa kuilinda na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.”, alifafanua Dkt. Shein.

0 maoni:

Chapisha Maoni