Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka  matarajio makubwa kwa Bodi ya Hospitali ya Mnazi mmoja katika kufanikisha azma  ya kuwa Taasisi yenye mfumo wa kujitegemea baada ya Baraza la Wawakilishi kupitisha Sheria ya kuanzishwa taasisi hiyo.
Amesema Bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti mzoefu wa masuala ya Afya Zanzibar Dkt. Abdulwakil Idrissa Abdulwakil inahitaji mashirikiano ya karibu ya  wafanyakazi wa Hospitali hiyo na wananchi katika Kuleta mabadiliko hayo.
Waziri Mahmoud ameeleza hayo Ofisini kwake Mnazimmoja alipokuwa akizindua Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Mnazi mmoja  ambayo lengo lake kuu ni kuifanya Hospitali hiyo  kufikia kuwa ya rufaa inayoshughulikia maradhi maalum yaliyoshindikana katika vituo vya afya na Hospitali za kawaida.
“Tunawataka  wananchi kutoa ushirikiano  kwa kuvitumia vituo vya afya vilivyo karibu nao, vinavyofikia 142, na kuiacha taasisi mpya ya Mnazi mmoja kushughulia magonjwa  makubwa,”alisisitiza Waziri wa Afya.
 Ameitaka Bodi  kuishauri Serikali njia bora za kuchangia matibabu katika maeneo maalum kwa vile Sera ya Serikali bado ni kuendelea kutoa matibabu bila malipo kwa wananchi.
Waziri wa Afya amewaeleza wajumbe wa Bodi hiyo kuwa  Hospitali ya Mnazi mmoja inarasilimali kubwa ya kuaminiwa na wananchi wengi wa Zanzibar na linapotokea tatizo lolote huwa ni la nchi nzima hivyo suala la kuongeza ufanisi lina  umuhimu mkubwa.
Amesema hivi karibuni Hospitali hiyo itafunga majengo mengine mawili mapya ambayo yanavifaa vya kisasa hivyo wafanyakazi watapaswa kuwa waangalifu na kuacha kufanyakazi kwa mazoea.
Amewataka viongozi wa sehemu zote za Hospitali ya Mnazimmoja kuwasimamia wafanyakazi walio chini yao na kuiunga mkono Bodi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Hospitali hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Abdulwakil Idrissa Abdulwakil amesema jukumu walilopewa na Serikali ni kubwa lakini kwa kutumia utaalamu wa wajumbe wa Bodi hiyo watajitahidi kuhakikisha malengo yaliyowekwa ya kuifanya Hospitali ya Mnazimmoja kuwa ya kujitegemea linafikiwa.
Hata hivyo amewaomba viongozi wa Wizara na wafanyakazi  wa Hospitali ya Mnazimmoja kuwapa ushirikiano na watakuwa tayari kupokea ushauri utakaosaidia  kufikia malengo yaliyopangwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili amewaeleza wajumbe wa Bodi ya Hospitali ya Mnazi mmoja kuwa Wizara itaendelea kusimamia sera lakini Bodi ndio yenye jukumu la kushauri maendeleo ya taaisi hiyo.
Na  Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar 
2Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja Dkt.Abdulwakil Idrissa Abdulwakil  akitoa shukrani kwa Waziri wa Afya  Mahmuod Thabit Kombo (hayupo pichani) baada ya kuzindua  Bodi hiyo.
21Waziri wa Afya Zanzibar Mahmuod Thabit Kombo akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Hospitali ya Mnazimmoja katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo iliyofanyika Wizara ya Afya Mjini Zanzibar.
3Waziri wa Afya Zanzibar Mahmuod Thabit Kombo katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Hospitali ya Mnazi baada ya kuizindua rasmi Bodi hiyo, wa kwanza (kushoto) Katibu Mkuu Wizara ya Afya Jama Malik Akili na (kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Abdulwakil Idrissa Abdulwakil.
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.