Alhamisi, 3 Novemba 2016

HALMASHAURI YA MUFINDI YAKOPESHA MILIONI 150 KWA WANAWAKE NA VIJANA.

Posted by Esta Malibiche on Nov 3,2016 in NEWS

Na Esta Malibiche 
Mufindi

Jumla ya shilingi milioni 150 zimetolewa kwa sharti la mikopo kwa vikundi vya  wanawake na Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, ikiwa ni  asilimia 10 ya Fedha iliyokusanywa na halmashauri hiyo  kwa kipindi cha miezi mitatu tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2016 – 2017 mapema mwezi Julai mwaka huu.

Akizungumza na Wandishi wa Habari Ofisini kwake,Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Dkt. Riziki Shemdoe amesema jumla ya vikundi vilivyokopeshwa  fedha hizo ni 89 ambapo vikundi 42 ni vya vijana vikiwa na jumla ya shilingi milioni 75 wakati vikundi 58 ni vya wanawake navyo vimewezeshwa kiasi kama hicho.
Akibainisha vigezo sita  vilivyozingatiwa wakati wa utoaji wa mikopo hiyo, kuwa ni pamoja na uhai wa kikundi kinachoomba mkopo, uwepo wa katiba kwa kikundi husika, hati ya utambulisho ya kikundi, kiwango cha Fedha kinachoombwa kisizidi milioni 03, takwimu nzuri ya urejeshaji mikopo kwa vikundi vivyokopa siku za nyuma huku waombaji wote wakitakiwa  kupitisha maombi katika ngazi za vijiji na kata.
“Nataka kusisitiza kwa vikundi vyote vilivyopata mikopo hii na vitakavyo endelea kupata, ni lazima viatambue kuwa Fedha hizi hazitolewi kama mgao, Fedha hizi ni mkopo hivyo wale wote waliopata ni vema wazifanyie kazi kadri ya maandiko yaliyowasilishwa na endapo kikundi chochote kitaenda kinyume kitakuwa kimepoteza sifa ya kukopesheka kwa mara nyingine pia ofisi yangu haitasita kuchukua hatua za kisheria”
Dkt. Shemdoe ameongeza kuwa kabla ya kukabidhi hudi kwa vikundi hivyo, Ofisi yake itataoa mafunzo  maalum kwa vikundi vyote ili   kuvijengea uwezo wa kuendesha shughuli za kijasiriamali katika vikundi ili viweze kufanya shughuli hizo kwa mafanikio na kupata faida pamoja na kufanya marejesho kwa wakati ili fedha hizo na nyingine zitakazo endelea kutengwa zitumike kuvikopesha vikundi vingine katika robo inayofuata.
Aidha, Dkt. Shemdoe, ameahidi kuendelea kutenga asilimia 10 ya Fedha zitakazo endelea kukusanywa na halmashauri yake kwa ajili ya wanawake na vijana kwa kila robo huku akitoa rai kwa vikundi vingi zaidi kuendelea kuundwa na kukidhi sifa stahiki ili viweze kukoposhwa katika awamu zinazofuata.

0 maoni:

Chapisha Maoni