KONGAMANO kubwa la aina
yake limefanyika mjini Dar es salaam ambapo washiriki walizungumzia
namna ya kuendeleza rasilimali watu katika eneo la utaalamu na taaluma
katika shughuli mbalimbali za uendelezaji wa makampuni na viwanda.
Kongamano hilo ambalo
lilihudhuria na watu wenye kariba kubwa katika masuala ya viwanda na
biashara akiwemo Dkt. Reginald Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa makampuni
ya IPP na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF);na Balozi wa
Ufaransa nchini Malika Berak liliangalia uhaba wa wataalamu na namna ya
kuuondoa uhaba huo wakati taifa linaelekea katika uchumi wa kati
unaotegemea viwanda.
Wengine waliokuwepo katika
kongamano hilo Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Dkt. Tonia Kandiero na maofisa wa serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akikaribisha
washiriki na wadau wengine alisema kwamba mafunzo hayo yaliyoratibiwa
kwa pamoja katika wataalamu wa Ufaransa, ESRF na Benki ya Maendeleo ya
Afrika yamelenga kudadavua tatizo lililopo na kulipatia ufumbuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (katikati)
akisalimiana na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi
(TPSF), Dk. Reginald Mengi (kulia) alipowasili katika ofisi za ESRF
jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika
Berak.
Taasisi ya utoaji mafunzo ya
Ufaransa ya AFPA ndiyo ilikuwa inaendesha mafunzo hayo wakibadilishana
uzoefu na wadau wa Tanzania kutoka sekta binafsi.
Akifafanua zaidi Dkt. Kida
alisema kwamba kongamano hilo limelenga zaidi katika kubadilishana
uzoefu kuhusu changamoto zinazojitokeza na fursa zilizopo katika
mafunzo, ukuzaji na uendelezaji taaluma.
Dkt. Kida alifurahishwa na
mchanganyiko wa watu kutoka sekta binafsi waliofika katika kongamano
hilo ambao aliamini kwamba wataelezea uzoefu wao katika kukabiliana na
changamoto za taaluma katika makampuni yao.
Aidha alisema kwamba wadau hao
wa Tanzania watapata uzoefu wa timu ya wataalamu wanne kutoka kwa wakala
wa mafunzo ya taaluma nchini Ufaransa (AFPA) ambao wataeleza miaka 60
ya uzoefu katika masuala ya mafunzo ya taaluma na uendelezaji wa
utaalamu.
Balozi wa
Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak (kushoto) akibadilishana mawazo na
mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald
Mengi (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa
Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida katika ofisi za ESRF jijini
Dar es Salaam.
Alisema anaamini kwamba
mchanganyiko huo wa wadau utasaidia katika kukabiliana na tatizo la
taaluma katika soko la ajira la Tanzania.
Alisema mazungumzo hayo ni
muhimu sana katika kuibua fursa hasa wakati taifa hili linajipanga
kuelekea katika uchumi wa kati wa viwanda na bila wataalamu wenye
taaluma zao makamapuni na viwanda vingi vitakuwa na shida kubwa.
Alisema changamoto kubwa
inayokabili taifa la Tanzania kuelekea nchi ya viwanda kama ilivyo
katika nchi nyingine zinazoendelea ni ukosefu wa taaluma na utaalamu.
“Ukosefu wa wafanyakazi wenye
taaluma katika ngazi zote ni tatizo kubwa linalokabili harakati za
kuelekea uchumi wa viwanda” alisema Dkt. Kida.
Anasema pamoja na matatizo hayo
taasisi yake tayari imeshaanza kushughulikia shida hiyo ya taaluma
nchini Tanzania kwa kuwa na makongamano mbalimbali makubwa
yanayokutanisha wadau kuzungumzia hali hiyo.
Balozi wa Ufaransa nchini, Mh.
Malika Berak (kulia) akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero (kushoto) alipowasili
ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na
Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (katikati) kabla ya kuelekea kwenye
ukumbi wa mikutano.
Alisema kwa mfano mwaka 2015
iliendesha jukwaa la mafunzo ya ufundi (VTEC) Africa. Katika jukwaa hilo
lililofanyika Machi 10 -12 mwaka huo walizungumzia mafunzo ya utaalamu
wa gesi na mafuta kwa mataifa ya Afrika. Jukwaa hilo liliendeshwa kwa
kushirikiana na kampuni ya Uingereza ya Getenergy.
Aidha Oktoba 9, 2015 iliendesha semina kuhusu uumbaji wa programu za mafunzo kwa aili ya kupata wataalamu wa gesi na mafuta.
Lakini, alisema, kuanzia Julai
2014, ESRF imekuwa ikishirikiana na shirika la Maendeleo la Marekani
(USAID) kutekeleza mpango wa miaka mitano wa mafunzo ya kinadharia na
utaalamu yenye mfumo wa Ushiriki ambapo ESRF yenyewe hutoa msaada wa
kitawala na lojistiki kwa wanafunzi ili waweze kwenda kuhudhuria mafunzo
nje ya nchi.
Aidha ESRF imekuwa ikifanya
tafiti mbalimbali na uchambuzi kuhusiana na uendelezaji wa taaluma
nchini Tanzania na moja ya ya tafiti hiyo ni kudorora kwa ubora wa elimu
Tanzania na namna ya kuzuia anguko hilo na kulibadili.
Mwaka 2014 na mwaka huu kuna
mada inayozungumzia uendelezaji wa mafunzo ya taaluma na uwezo wa
uzalishaji Tanzania.Mada hii ni sehemu ya taarifa ambazo zitapatikaa
katika ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2017.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kulia)
akiongozana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Dkt. Tonia Kandiero kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano wa ESRF. Nyuma ni
Balozi wa Ufaransa nchini, Mh. Malika Berak akibadilishana mawazo na
mgeni rasmi Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Reginald
Mengi pamoja na Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ally Msaki.
Continue reading →