Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhuru
Music (T) Ltd, Maneno Sanga (kulia), akiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya
Hualang Electric ambao ndio watengenezaji wa vyombo vya muziki vya
Candy, Yang Hongwei wakati wa kusaini mkataba wa kibiashara wa kusambaza
vyombo vya muziki na matangazo vya kampuni hiyo kwa nchi za tano za
Afrika Mashariki.
Baadhi ya vyombo vya muziki na matangazo vya Candy ambavyo vinasambazwa nchini na kampuni ya Uhuru Music (T) Ltd.
……………………………………………………………………………
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Kampuni ya kusambaza vifaa vya
muziki na matangazo ya Uhuru Music (T) Ltd, ya jijini Dar es Salaam,
imewaonya matapeli wanaoghushi nembo ya vyombo vya muziki na matangazo
vya Candy kuwa siku zao zinahesabika na wakati wowote watakumbana na
nguvu za dola baada ya mbinu wanazotumia kufanya utapeli huo kubainika.
Taarifa kwa vyombo vya habari
iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Maneno Sanga ilisema
kuwa kikosi kazi cha kampuni hiyo kimegundua njia wanazotumia matapeli
hao ambao ni pamoja na kutengeneza vyombo vya muziki na matangazo nchini
kwa kutumia teknolojia duni na kubandika nembo bandia ya Candy.
Alibainisha kuwa maharamia hao
ambao wana karakarana zao katika maeneo ambayo wameisha yabaini,
wamekuwa wakiharibu sifa ya bidhaa hizo ambazo zinatengenezwa na kampuni
ya Hualang Electric Company Ltd ya China.
“Uhuru Music (T) Ltd, ndio ambao
tuna mkataba wa kusambaza vyombo vya muziki na matangazo vya Candy kwa
nchi tano za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania na sio vinginevyo”
alisema na kuongeza kuwa pia kuna mawakala ambao wana mikataba na
kampuni yake katika kanda tofauti nchini.
Alisema wamewasiliana na mamlaka
zote ikiwa ni pamoja na vyombo vya usalama kuhusiana na uhalifu huo
ambao pia unaikosesha serikali mapato na kuwatia hasara wananchi kwa
kuwauzaia vifaa visivyo na ubora unaotarajiwa.
Anataka watu ambao wanahitaji
kununua vifaa vya muziki vya Candy kujiridhisha kwanza kabla ya kufanya
manunuzi kwa kuangalia alama tatu muhimu ambazo zinavitambulisha vyombo
hivyo ikiwa ni pamoja na ile ambayo ipo katika nembo ya kampuni hiyo
ambayo ni kama iliyopo katika fedha za noti.
“Katika logo ya Candy ukiangalia
vizuri kuna alama ya fedha ambayo inabadilika badilika na kusomeka
maandishi Candy American Technology” anasema na kuongeza kuwa kama
bidhaa hiyo ya Candy katika nembo yake haina hiyo chombo hicho ni feki.
Anasema utambulisho mwingine
unapatikana kupitia simu ya mkononi aina za Smart kwa mteja ku-scan
alama ya siri ya biashara (Barcode) ambayo inapatikana katika bidhaa
hizo na kumletea taarifa zote ikiwa ni pamoja na jina la kampuni yake ya
Uhuru Music (T) Ltd.
Pia anabainisha kuwa nembo (logo)
za Candy ni za chuma na wala si plastiki kama zilivyo hizo za feki
hivyo ni wajibu wa wateja kuzitambua alama hizo na kukataa kufanywa
dampo la bidhaa feki ninyingi ni hafifu na zisizodumu katika matumizi.
Anasema wameamua kutoa ufafanuzi
huo na kuunda kikosi kazi cha kuchunguza uharamia unaofanyika baada
kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja ambao wamenunua ala za
muziki zenye nembo ya Candy kwa bei ya chini, mbaya zaidi havikuwa na
ubora unaotakiwa.
“Tulipofuatilia tulibaini
wanapotengenezea, mbinu wanazotumia kuwahadaa wateja na tumeshirikisha
mamlaka zingine wakati wote wa ufuatiliaji” anasema na kuongeza kuwa
kuanzia sasa kinachofuata ni hatua za kisheria.
Anazitaja vyombo hivyo vya muziki
na matangazo kuwa ni pamoja na vipaza na vinasa sauti, vyombo vya
matangazo, spika, mic kwa ajili ya kurekodi muziki, vinanda, stendi
maalum za kurekodia, vyombo vya matangazo katika magari na Deck za aina
mbalimbali.
Pia taa kwa ajili ya kumbi za
disco, vifaa vya kuchanganyia muziki, vifaa vya studio kwa ajili ya
kurekodia na bidhaa zingine ambazo zinahusiana na masuala ya muziki na
matangazo.
Uhuru Music (T) Ltd, ndio wenye
mkataba pia wa kusambaza vyombo hivyo vya muziki na matangazo katika
nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.