Wizara ya Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari juu ya ugonjwa wa homa ya
manjano ambao umethibitika kuwepo nchi ya jirani ya Kenya.
Tahadhari hiyo imetolewa leo
Jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokua akiongea na waandishi wa habari
kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu nchini ambapo katika wiki ya
tarehe 14 Machi hadi 20 Machi mwaka huu takwimu zinaonyesha kuwa kati
ya Mikoa 13 yenye wagonjwa wa kipindupindu , jumla ya wagonjwa 738 na
vifo 16 vimeripotiwa huku Mkoa wa Manyara ukiongoza kwa kuwa na
wagonjwa wengi wa kipindupindu.
Akielezea kuhusu ugonjwa wa homa
ya manjano,Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa ugonjwa huu unasababishwa na
virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes na baadhi ya dalili zake
ni homa, kuumwa kichwa,maumivu ya misuli na mgongo,kupoteza hamu ya kula
pia kutoka damu sehemu za mwili zilizo wazi.
“Wizara inapenda kutoa tahadhari
ya ugonjwa wa homa ya manjano kwa wananchi wote na hasa wanaokaa
mipakani mwa nchi ya Kenya kwa kuwa ugonjwa huu hauna tiba kamili ila
una chanjo, mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zinazojitokeza ikiwa ni
pamoja na kupewa dawa za kushusha homa, maumivu, kuongezewa maji
mwilini kwa kunywa au kuwekewa dripu”alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewaagiza
Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kupambana na magonjwa ya
kuambukiza kwa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa wagonjwa na utaratibu
wa utoaji taarifa za magonjwa ya kuambukiza, kuhakikisha wasafiri
wanaoingia na kutoka nchi zenye hatari ya ugonjwa huo wanapewa chanjo
kabla ya kuingia nchi nyingine, kutoa elimu ya afya kwa wananchi,
kuandaa timu za wataalam, vifaa tiba na chanjo za kutosha ili kuweza
kukabiliana na ugonjwa huo endapo utajitokeza nchini kwa kusimamia na
kuhimiza usafi wa mazingira na kuzingatia kanuni za afya.
Pia,amewaonya maofisa wanaotoa
chanjo ya homa ya manjano walioko katika vituo vya Afya vya kupokelea
wageni wanaoingia na kutoka nchini kuacha mtindo wa kupokea rushwa na
kuwapitisha watu bila kupatiwa chanjo.
Mwisho, ametoa wito kwa wananchi
kuchukua tahadhari na kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa afya
walioko katika maeneo yao kwa kutoa taarifa haraka kwenye uongozi
husika endapo kuna mgonjwa mwenye dalili za kipindupindu au homa ya
manjano.
0 maoni:
Chapisha Maoni