Jumatano, 16 Machi 2016

KANGOYE ACHANGIA UKARABATI WA JENGO LA CCM LILILOWAKA MOTO


KADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya KANMAR Ltd, Jackson Kangoye ametoa mchango wa Sh 500,000 taslimu kusaidia ukarabati wa jengo la Ofisi za CCM Mkoa wa Manyara lililoungua moto hivikaribuni.
Jengo hilo lililopo eneo la kata ya Bagara mjini Babati, liliungua kwa moto huo Machi 7, mwaka huu majira saa 1:30 usiku.
Akikabidhi mchango huo kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndengiaso Ndekubali; Kangoye aliwapa pole wana CCM wa mkoa huo akisema kuna mambo mengi yatakuwa yamerudi nyuma baada ya jengo hilo kuungua kwa moto.
Kangoye alisema kama mwana CCM wa kawaida ameguswa na ajali hiyo ya moto na kuamua kuchangia kiasi hicho cha fedha huku akiwahamasisha makada wengine kujitokeza kuisaidia CCM Mkoa wa Manyara kwa hali na mali.
“Ili kuendelea kuiimarisha CCM, wana CCM tuna wajibika kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kujitolea yanapotokea majanga kama haya,” alisema.
Akishukuru kwa msaada huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara alisema utataumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
“Nimshukuru Kangoye kwa mchango wake, ni imani yangu kwamba wana CCM wengine wa ndani na nje ya mkoa wa Manyara watatuunga mkono ili tuweze kuirudisha ofisi yetu katika hali yake ya kawaida,” Ndekubali alisema.
Wakati baadhi ya watu wakiamini chanzo cha moto huo ni itilafu ya umeme iliyotokea katika moja ya vyumba vyake, katibu huyo alisema chanzo cha moto huo uliounguza mali mbalimbali zilizokuwamo kwenye jengo hilo la ghorofa moja lenye vyumba 20, bado kinachunguzwa.
Miongoni mwa ofisi zilizoteketea ni ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Lucas ole Mukus, katibu wa mkoa, mwenyekiti wa UVCCM, Regina Ndege na ofisi za jumuiya za UWT na wazazi.

Pichani
Katibu wa CCM MKoa wa Manyara, Ndengiaso Ndekubali (katikati mbele) akimuonesha Jackson Kangoye  baadhi ya vyumba vya jengo la CCM la mkoa huo ambalo hivikaribuni lilitekekea kwa moto

0 maoni:

Chapisha Maoni