Alhamisi, 17 Machi 2016

Wakazi wa Wazo wamkuna Kamishna Sirro









AMISHNA Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amewapongeza wakazi wa Kata ya Madale Manispaa ya Kinondoni baada ya kufanikisha ujenzi wa kituo cha polisi cha kisasa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho hivi karibuni kilichopo katika kata ya Madale, Sirro alisema kuwepo kwa kituo hicho ni wazi kuwa vitendo vya uhalifu katika eneo hilo vitaisha. Kituo hicho ambacho kimejengwa na wananchi hao, kimegharimu zaidi ya Sh milioni 151 na kwamba kinatarajia kuanza kazi Aprili mosi mwaka huu.
“Kutokana na juhudi kubwa mlizozionesha katika ujenzi wa kituo hiki, jeshi kupitia Wizara husika (Mambo ya Ndani ya Nchi) linawapongeza kwa hatua mliyofika kwa sababu ni jambo kubwa mlilofanya,” alisema Sirro.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kituo hicho, Ladislaus Chang’a alisema kituo hicho kimejengwa kwa michango ya hiari iliyochangwa na wananchi wa mitaa mitano iliyopo katika Kata ya Madale na kwamba ndio iliyofanikisha ujenzi wa kituo hicho.
Alisema kituo hicho cha Polisi kina vyumba vitatu vya kuhifadhia mahabusu vilivyojengwa kwa kisasa ambapo kila chumba kina choo, bafu na maji ndani yake na kwamba vyumba hivyo vimetengwa tofauti kwa maana kuna chumba kwa ajili ya watoto, wanawake na wanaume.
“Tunaomba kituo hiki kiwe cha wilaya kwa sababu kimejengwa katika hadhi ya kitaifa na hakuna kituo cha polisi katika mkoa huu chenye chumba cha mahabusi ambacho ndani yake kuna huduma ya maji, choo na bafu yaani ndani kwa ndani... hata uende wapi huwezi kukuta huduma hii katika kituo cha polisi,” alisema Chang’a.

0 maoni:

Chapisha Maoni