KLABU ya Yanga imetaja viingilio vitakavyotumika katika mchezo ujao wa marudio klabu wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya APR utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi, ambapo kiingilio cha chini ni Sh 5,000 na cha juu Sh 25,000.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa Sh 5,000 kitatumika katika viti vya machungwa, kijani na bluu ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi kujitokeza kuishangilia timu hiyo.
Pia, alisema Sh 20,000 ni kwa ajili ya VIP B na C huku Sh 25,000 ikiwa ni VIP A na wakati huo huo, akihimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi siku hiyo kuishangilia timu yao. “Tunatambua mchango na thamani ya mashabiki wetu ndio maana tumeweka kiingilio kidogo kwa viti vingi ili washiriki kikamilifu,”alisema.
Kuelekea katika mchezo huo, Muro alisema maandalizi yanakwenda vizuri, ambapo wachezaji bado wako kambini hadi Ijumaa kujiimarisha. Alisema wamejipanga kushinda katika mchezo huo, na kwamba kwa sasa hawana mpango wa kuzungumzia ratiba ya ligi kwani wako katika maandalizi mazito ya mechi ya kimataifa hawataki kuvurugwa kisaikolojia.
Simba jana walidai kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa likipangua ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara mara kwa mara ili kuzibeba Yanga na Azam FC. Muro alihimiza makampuni ya ndani na nje yanayotaka kurusha matangazo ya mchezo huo kujitokeza ili kufanya mazungumzo.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Rwanda, Yanga ilishinda 2-1. Kwa mujibu wa Muro iwapo itafanikiwa kuifunga APR katika mchezo huo wa pili huenda ikaweka kambi Ulaya kujiandaa na mechi inayofuata ya kimataifa.
0 maoni:
Chapisha Maoni