MENEJA wa Ranchi ya Mifugo ya Missenyi mkoani Kagera anatuhumiwa kuhongwa Sh milioni 14.4 na mdogo wa kiongozi wa juu serikalini nchini Uganda kuingiza mifugo yake katika ranchi hiyo mali ya serikali.
Hata hivyo, alisema siku moja baada ya kutembelea ranchi hiyo yenye ukubwa hekta 60,851, alitumiwa ujumbe na aliyemtaja kuwa mdogo wa kiongozi wa Uganda akilalamikia hatua hiyo, akidai kumpa fedha meneja wa ranchi ili ng’ombe wake waingie humo.
“Nimepata ujumbe kutoka kwa mdogo wa kiongozi wa Uganda. Analalamika. Lakini katika hili, hakuna kinga. Kila mtu atawajibika kwa shughuli zake. Na serikali hii haihitaji sijui ni mdogo wa kiongozi, mjomba, sijui mtoto,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Alieleza kuwa katika hilo, mdogo huyo alidai kumpa Meneja wa Ranchi ya Missenyi Sh milioni 14.4 katika awamu tatu, tuhuma ambazo sasa amemuagiza Kaimu Mkuu wa Mkoa, Jackson Msome kuzichunguza. “Kama hili lina ukweli lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe. Nakuagiza Mkuu wa mkoa kurudi Missenyi kuchunguza hili na kama ukithibitisha, nategemea utachukua hatua kali za kinidhamu,” alieleza Waziri Mkuu.
Bila kutaja jina, Waziri Mkuu alisema mtumishi huyo wa umma anatuhumiwa kuhongwa fedha hizo katika awamu tatu; Sh milioni saba, milioni 3.5 na milioni nne. “Jana (Jumanne) nilipokuwa Missenyi nilipata fursa ya kutembelea Ranchi ya Missenyi pamoja na kukagua mpaka kati ya nchi ya Tanzania na Uganda. Huko niligundua kuna tatizo la matumizi ya ardhi,” alisema.
“Kuna wavamizi haramu wamevamia katika ranchi. Sio watanzania, hivyo nimeagiza wanyang’anywe ardhi hiyo, utaratibu wa kupata ardhi utaandaliwa upya,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa .
Alirejea kauli yake aliyoitoa alipotembelea ranchi hiyo kwamba wavamizi wote wa kigeni waliomo ndani ya ranchi hiyo na ile ya Kitengule, Karagwe, waondoke mara moja kurejea makwao hata kama wanamiliki vitalu.
Aliongeza, “nimeziagiza Kamati za Ulinzi za Usalama za Wilaya kwa kushirikiana na Mkoa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wizara husika kunyang’anya pia watu ambao hawajaendeleza vitalu vyao.” “Katika mapitio, tunataka kujua mmiliki wa kitalu ni nani, ni raia wa wapi, anaifanyia nini ardhi hiyo kama alivyopewa.
Na jambo hili lifanywe kwa haraka na umakinimakubwa,” aliagiza Waziri Mkuu. Wakati wazira yake, alielezwa na wananchi kuwa wapo wahamiaji haramu kutoka nchi jirani za Uganda na Rwanda waliomilikishwa vitalu katika ranchi hizo huku Watanzania wakinyimwa fursa ya kutumia ardhi hiyo.
Waziri Mkuu aliwatuhumu watendaji wa serikali kwa kurubuniwa na kuwaruhusu wageni kuingia nchini kiholela, na kuonya kuwa kamwe hawatavumiliwa. Lakini pia aliwalaumu Watanzania kwa kuzembea katika kulinda rasilimali zao na wengine kushiriki katika kugawa ardhi bila kujali athari zake kubwa kwao na kwa Taifa.
Mkoa wa Kagera una ranchi tano za Taifa za mifugo zinazomilikiwa na Shirika la Ranchi za Taifa (NARCO) zenye ukubwa wa jumla ya hekta 179,967.
0 maoni:
Chapisha Maoni