Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa tukio la kunajisiwa kwa watoto watatu wa kike wenye umri kati ya miaka minane hadi tisa, wanafunzi wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Msaranga manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambao limeripotiwa na vyombo vya habari.
Tukio hili la kunajisi watoto ni
ukiukwaji mkubwa wa haki za mtoto ambao Serikali imekuwa ikihimiza
wazazi, walezi, na jamii kuhakikisha kuwa mtoto analelezwa na
kuendelezwa katika mazingira salama na rafiki kwa mujibu wa Sheria ya
Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.
Wizara imesikitishwa na taarifa
kuwa, kuna baadhi ya wanajamii wanaowafanyia ukatili watoto wa kike kwa
kuwashurutisha kuwa na mahusiano na watoto hao katika umri mdogo,
kitendo ambacho kwa kiasi kikubwa kinarudisha nyuma jitihada za Serikali
kuhakikisha kuwa jamii zetu zinakuwa mahala salama kwa watoto kuishi.
Wizara inalaani vikali
unyanyasaji waliofanyiwa watoto hao kwani katika umri huo mdogo
hawakustahili kufanyiwa ukatili huo. Aidha, wazazi na walezi tutambue
kuwa tunaowajibu mkubwa wa kufuatilia mienendo ya watoto wetu mara kwa
mara ili kuwanusuru na matukio ya ukatili.
Wizara inatoa pongezi ya dhati
kwa wananchi, Jeshi la Polisi, wanahabari na wadau wote ambao wameonesha
ushirikiano kuripoti na matukio ya ukatili dhidi ya watoto hapa
nchini. Aidha, Wizara inapongeza Jeshi la Polisi katika Mkoa wa
Kilimanjaro kwa kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja anayehusishwa tukio
la kunajisi watoto hao. Tunahimiza Polisi katika mkoa wa Kilimanjaro
kumsaka mtuhumiwa wa pili na kumjumuisha katika shauri hili.
Maagizo yanatolewa kwa Mganga
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha anatoa huduma stahiki ya vipimo
na tiba kuokoa afya za watoto hao. Aidha, Afisa Ustawi wa Jamii na Afisa
Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Kilimanjaro wahakikishe wanafuatilia
shauri la watoto hawa kwa karibu, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya afya
za watoto hao; na kutoa ushauri nasaha kwa watoto, wazazi na walezi wa
familia za watoto hao na kutoa taarifa mara kwa mara.
0 maoni:
Chapisha Maoni