Jumatano, 16 Machi 2016

MBUNGE CHUMI ATOA WITO KWA JAMII KUSAIDIA SHULE YA WALEMAVU MAKALALA

Mbunge  wa  jimbo la Mafinga mjini Bw Cosato Chumi  akizungumza na  wanafunzi wakati wa ziara  yake ya  kikazi    
Mbunge  wa  jimbo la Mafinga mjini Bw Chumi akimsaidia mwanafunzi  mwenye  ulemavu wa ngozi albino  kuvaa kofia

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini wilayani Mufindi  mkoani Iringa Bw Cosato Chumi ametoa  wito kwa watu mbalimbali kuguswa na matatizo ya wanafunzi na shule Msingi ya Walemavu ya Makalala kwa kuchangia kile walichonacho ili changamoto zilizopo  kumalizika 
 
Mbunge   huyo  alitoa wito  huo  wakati wa ziara  yake ya  kutembelea  shule  na miradi mbali mbali katika   jimbo  hilo.
 
 
Alisema  iwapo  jamii  itaguswa na  kujitolea  kwa ajili ya wanafunzi hao  upo  uwezekano mkubwa wa wanafunzi hao  kusoma kwa furaha  zaidi na maendeleo yao kitaaluma  kuboreshwa .
 
Hata  hivyo kuhusu uhaba wa walimu na mabweni Bw Chumi alisema serikali inatakiwa kuitazama shule hiyo kwa jicho la huruma ili mahitaji hayo yapatikane.
“Shule inahitaji mabweni ya ziada na yaliyopo yakarabatiwe; wito wangu kazi hii isiachwe kwa serikali pekee yake, tunaomba wadau wetu wajitokeze kusaidia kuboresha miundombinu hiyo na kushughulikia changamoto zingine,” alisema.
Shule hiyo inayochukua wanafunzi wasioona na wenye ulemavu wa akili kutoka maeneo mbalimbali nchini ilianzishwa mwaka 1954. Shule  hiyo  iliyopo  nje  kidogo na mji  wa mafinga   inahitaji  serikali na wadau wake kuinusuru ili kuwatenda haki wanafunzi wanaosoma na wanaohitaji kujiunga nayo.
Shule hiyo ina  jumla ya wanafunzi 79, ina mwalimu mmoja tu wakati mahitaji ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano.
 
Mkuu wa shule hiyo, Shem Muheni alisema haina mabweni ya kutosha jambo lililosababisha ishindwe kupokea wanafunzi wengi waliotaka kujiunga mwaka huu.
“Wanafunzi wengi wako nyumbani, tunashindwa kuwapokea kwasababu ya uhaba wa mabweni, hapa tuna mabweni mawili tu kwa wanafunzi wa kike na kiume ambayo hayakidhi mahitaji ya wanafunzi waliopo,” alisema.
Alisema miundombinu ya mabweni hayo ni ya zamani kwani mbali na kutokuwa rafiki kwa wanafunzi hao wakati wakitoka na kuingia ndani, madirisha yake hayafunguki na yana vitanda vichache ambavyo havikidhi mahitaji.
Wakati shule hiyo ikiwa katika wilaya inayoongoza kwa kuwa na misitu ya kupandwa nchini(msitu wa Taifa wa Saohill), Muheni alisema wanafunzi hao wanalala wawili badala ya mmoja kwa kila kitanda huku bwalo la chakula likiwa na meza nne tu wakati mahitaji ni zaidi ya meza kumi.
“Lakini pia hawana nguo, viatu na vifaa vya kujifunzia ambavyo havitoshelezi mahitaji yao ya kila siku,” alisema.
Kuhusu chakula, Muheni alisema pamoja na kwamba serikali imekuwa ikitekeleza wajibu wake wa kupeleka chakula shuleni hapo hasa unga na maharege, wanafunzi hao wanahitaji kula vyakula mchanganyiko ili kukidhi mahitaji yao ya mwili na akili.
 

0 maoni:

Chapisha Maoni