MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imefungia akaunti ya facebook na tovuti
ya www.focusvikoba. wapka.mobi, iliyoanzishwa na matapeli wa mtandao
wakidai ni ya Mke wa Rais, Mama Janet Magufuli na kuomba wananchi kutuma
fedha za kiingilio kwa Vicoba ili wapate mikopo.
Taarifa
ya TCRA iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa uchunguzi
wa mamlaka hiyo, umeonesha kwamba Mama Magufuli hana akaunti ya Facebook
wala tovuti inayohamasisha watu kuomba mikopo ya vikundi vya Vicoba.
Mkurugenzi
Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba amesema katika taarifa hiyo kwamba akaunti
hiyo ya Facebook iliyodaiwa kuwa ni ya Mama Janet, ilianzishwa na
matapeli wa mtandao.
Dk Simba
alisema ingawa kumekuwepo na maendeleo na mabadiliko makubwa katika
sekta ya mawasiliano nchini Tanzania, kuongezeka kwa idadi ya watoa
huduma za mawasiliano, idadi ya watumiaji na aina ya huduma
zinazotolewa, lakini kuna wachache wanaotumia huduma hivyo kutenda
uhalifu.
Kwa
mujibu wa Dk Simba, wahalifu hao hutumia simu za mkononi na kwenye
intaneti kuanzisha tovuti za kihalifu na kupitia mitandao ya kijamii
kama vile Facebook. Alisema hivi karibuni kumekuwa na matukio ya
wahalifu wa mtandao kuanzisha tovuti na blogu na pia kurasa za facebook
kwa kutumia majina ya viongozi wakuu wa nchi, wabunge na watu wengine
maarufu.
Wahalifu
hao kwa mujibu wa taarifa hiyo, hudanganya wananchi kwamba kuna fursa za
kupata mikopo au misaada kupitia vikundi vya kusaidiana, maarufu kama
Vicoba na kuwataka wananchi watume fedha za kujiunga na huduma hizo kwa
njia za simu za mkononi.
Alisema
pamoja na kuzifungia akaunti hizo za facebook na tovuti, Mamlaka
inashirikiana na Polisi kuchunguza matukio hayo na tayari hatua kubwa
imefikiwa katika kuwakamata na kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya
sheria.
Mkurugenzi
Mkuu huyo amesema kwa mujibu wa kifungu cha 15 (1) cha Sheria ya Makosa
ya Mtandao ya 2015, mtu yeyote haruhusiwi, kwa kutumia kompyuta,
kujifanya yeye ni mtu mwingine.
Adhabu
kwa kutenda kosa hili kwa mujibu wa Dk Simba, imeainishwa kwenye kifungu
cha 15 (2) ambacho kinasema mtu akipatikana na hatia anaweza kutozwa
faini isiyopungua Sh milioni 5 au mara tatu ya thamani ya kile
alichopata kupitia ulaghai huo, au kiasi ambacho ni kikubwa kati ya
faini na mara tatu ya alichokipata.
Mke wa Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzani,mama Janeth Magufuli
0 maoni:
Chapisha Maoni