Jengo la Mahakama Kuu. ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATCL) David Mattaka, na wenzake wawili, wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 86.5. Mattaka anadaiwa kusababisha hasara hiyo kutokana na kusaini mkataba wa kukodi ndege bila kufuata.
ALIYEKUWA
Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATCL) David Mattaka, na wenzake wawili,
wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya
madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 86.5.
Mattaka
anadaiwa kusababisha hasara hiyo kutokana na kusaini mkataba wa kukodi
ndege bila kufuata Sheria ya manunuzi ya umma pamoja na ushauri wa
kiufundi. Mbali na Mattaka washtakiwa wengine waliofikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Ramadhani Mlinga pamoja na
Mkurugenzi wa Sheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.
Washtakiwa
hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashitaka sita na Wakili
wa Serikali Mkuu, Vitalis Timony pamoja na mawakili kutoka Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Peter Vitalis na Stanley Luoga
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Respicius Mwijage.
Wakili
Timony alidai kuwa, Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL Dar es Salaam,
Mattaka akiwa Mkurugenzi wa shirika hilo, alitumia madaraka yake vibaya
kwa kusaini makubaliano ya kukodi ndege yenye namba A 320-214, kati ya
ATCL na kampuni ya Wallis Trading Inc, bila kufuata sheria ya manunuzi
ya umma na taratibu za zabuni.
Aliendelea
kudai kuwa, Oktoba 27, 2007, Mattaka alitumia madaraka vibaya kwa
kusaini makubaliano ya kukodi ndege hiyo bila kufuata ushauri wa
kiufundi. Katika mashitaka mengine, inadaiwa kati ya Oktoba 27, 2007 na
Aprili 24, 2008, Mattaka alisaini makubaliano hayo bila kufuata ushauri
wa kiufundi jambo ambalo lilisababisha shirika hilo kupata hasara ya
dola za Kimarekani 772,402.08 ambazo zililipwa kwa kampuni ya
Aeromantenimiento kama gharama ya matengenezo ya ndege hiyo.
Aidha
inadaiwa kati ya Oktoba 27 na Novemba 29, 2007, Mattaka aliidhinisha
makubaliano hayo bila kufuata ushauri wa kiufundi na kusababisha hasara
ya dola za kimarekani 35,984.82, ambazo zililipwa kwa kampuni ya Lantal
textiles kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali vya ndege hiyo.
Wakili
Timony aliendelea kudai, kati ya Oktoba 27, 2007 na Oktoba 26, 2011, kwa
kutumia madaraka yake vibaya, Mattaka aliidhinisha makubaliano hayo na
kuisababishia serikali hasara ya dola za Kimarekani 42,459,316 ambazo
ATCL iliilipa kampuni ya Wallis Trading Inc.
Katika
mashtaka yanayowakabili, Mlinga na Soka, inadaiwa Machi 19, 2008, katika
ofisi za PPRA, Ilala Dar es Salaam, kwa lengo la kufanya udanganyifu,
walighushi muhtasari wa kikao cha Machi 19, 2008, kwa lengo la kuonesha
siku hiyo, PPRA ilifanya kikao kujadili maombi ya kuruhusu makubaliano
ya ATCL kukodi ndege.
Baada ya
kusomewa mashitaka, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama
Kuu. Wakili Timony alidai upelelezi wa kesi bado unaendelea, pia hawana
pingamizi la dhamana kwa Mlinga na Soka kwa kuwa shitaka linalowakabili
lina dhamana.
Hata
hivyo alidai wanapinga dhamana ya Mattaka kwa kuwa mahakama hiyo haina
mamlaka ya kutoa dhamana kwa mashtaka ya Uhujumu Uchumi pia mashitaka
yanayomkabili yanahusisha zaidi ya Sh bilioni 10, hivyo alishauri
awasilishe maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu.
Mlinga na
Soka waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na
mdhamini mmoja alisaini hati ya Sh milioni 10, Mattaka alirudishwa
rumande. Hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 29 mwaka huu
itakapotajwa tena.
0 maoni:
Chapisha Maoni