Alhamisi, 17 Machi 2016

MAMA SAMIA,VIFO VYA AKINA MAMA HAVIVUMILIKI






Makamu wa Rais SAMIA  HASSAN SULUHU akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya utepete mweupe na uzinduzi wa kampeni ya vifo vya mama vitakanavyo viwanja vya karimjee jijini Dar es salaam jana.


MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu amesema vifo vitokanavyo na uzazi havivumiliki hivyo serikali sanjari na wadau mbalimbali wanawajibika kuvikomesha. Alisema hayo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe yaliyofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam.

Yaliongozwa na kauli mbiu ya ‘Vifo vitokanavyo na uzazi havivumiliki, wajibika’. Mama Samia ambaye alieleza kuunga mkono kauli mbiu hiyo, alisema Serikai inatambua changamoto hii, na imejipanga kukabiliana nayo, ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa maendeleo ya afya ya msingi, ambao shabaha yake ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati na pia kila kata inakuwa na kituo cha afya.

Alisema lengo ni kuhakikisha tiba na huduma za watoto, zinapatikana kwa urahisi. Alisema chini ya mkakati wa kupunguza vifo vya wajawazito, watoto wachanga na walio chini ya umri wa miaka mitano, wanataka angalau asilimia 50 ya vituo vyote vitoe huduma ya upasuaji na damu salama.

Alizitaka halmashauri katika mipango yao ya bajeti ya mwaka 2016/17, zihakikishe zinajiwekea lengo la kuhakikisha hospitali za wilaya zinakuwa na huduma kamili za uzazi salama kwa asilimia 100.

Awali, Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe na Uzazi Salama Tanzania (WRAT), Rose Mlay, aliiomba serikali kutenga bajeti ya kutosha kuhakikisha kila kituo cha afya, mjamzito anapokwenda anapata mahitaji yote ya muhimu ya kumwezesha kujifungua salama.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Mganga Mkuu, Profesa Muhammed Bakari alisema wanawake 24 hupoteza maisha kila siku na wengine 30 huponea chupuchupu ikiwemo kupata ulemavu kutokana na matatizo ya uzazi.

0 maoni:

Chapisha Maoni