Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mawakala wa Forodha na Bandari kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam Machi 21, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Amtaka Mkurugenzi wa Bandari aandae dispatch zote tangu 2014
Naibu Waziri Ujenzi aagiza kampuni za forodha zifunguliwe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali aende Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) ili akague taarifa za mapato ambazo zilikuwa zikilipwa
na mawakala wa forodha na bandari kupitia benki ya CRDB lakini
hazionekani kwenye mifumo ya benki.
Ametoa agizo hilo leo jioni
(Jumatatu, Machi 21, 2016) wakati akizungumza na mamia ya mawakala wa
forodha na bandari waliohudhuria mkutano aliouitisha ili kusikiliza kero
zinazowapata katika utendaji kazi wao.
Akizungumza na mawakala hao kwenye
ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema kuna
dalili za kutupiana lawama baina TPA na CRDB kuhusu malipo yaliyikuwa
yakifanyika benki halafu fedha hazionekana na wakala anaidaiwa kuwa
hajalipia mzigo wakati alishaulipia.
“Kimsingi bado liko tatizo baina
ya Mamlaka ya Bandari pamoja na Benki ya CRDB. Naona kila mmoja hapa
anamkana mwenzake. Nitamtuma CAG ili akafanye ukaguzi wa kina ili tujue
ni nani kati yao amehusika na upotevu wa fedha,” alisema huku
akishangiliwa na mawakala hao.
Alimwagiza pia Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei aandae dispatch
zote walizotumia kupokelea malipo za kuanzia mwaka 2015 na ikibidi
aandae za kuanzia mwaka 2014 ili CAG anapozopitia aweze kupata picha
halisi.
Vilevile, Waziri Mkuu alimwagiza
Eng. Matei kuhakikisha wananunua mashine ya photocopy ili iwekwe kwenye
chumba cha kupokelea stakabadhi za malipo ya benki (bank pay in slip)
ili mteja anapoleta nakala ya benki aweze kutolewa photocopy na kubakia
na nakala ya malipo aliyofanya,
Waziri Mkuu alisema Serikali
inatambua bandari ni eneo nyeti katika kuinua uchumi na mapato ya nchi
lakini pia ni eneo muhimu katika kutengeneza ajira. “Ninapenda
niwahakikishie kuwa bado tutaendelea kukagua bandari hadi pawe safi. Hii
bandari ni yenu na mtafanya kazi kama kawaida,” alisema.
Mapema, akizumgumza kwa niaba ya
mawakala hao, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha nchini (TAFFA), Bw.
Stephen Ngatunga alieleza matatizo mbalimbali ambayo wao kama mawakala
wa forodha wamekuwa wakikumbana nayo kuanzia ulipaji, utoaji wa mizigo
na kuitaka Serikali iongeze nguvu katika kuikabilia sekta hiyo.
Alizikosoa baadhi ya sheria ambazo
zinaruhusu wamiliki wa bandari kavu kumiliki pia makampuni ya uwakala
wa forodha, sheria kadhaa zinazochangia kukwamisha utoaji wa mizigo
bandarini, ukaguzi hafifu wa kwenye scanner na uwepo wa vituo vinane vya
mizani kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma ambavyo vimegeuka kuwa kero
kwa wasafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani amesema Serikali
imeamua kuyafungulia makampuni zaidi ya 150 ambayo yalikuwa yamefungiwa
kufanya kazi za uwakala wa forodha kutokana na madai ya kuhusishwa na
ukwepaji wa kodi.
“Hapa tumegundua kuwa wote siyo
wasafi iwe ni mawakala, benki ama bandari. Mkurugenzi wa Bandari,
kuanzia leo watu hawa waruhusiwe waanze kufanya biashara lakini nyaraka
za nyuma zisiguswe hadi CAG atakapokamilisha uchunguzi wake,” alisema
kuibua kelele za shangwe kwenye ukumbi huo.
IMETOLEWA NA OSIFI YA WAZIORI MKUU
0 maoni:
Chapisha Maoni