NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi,
Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jaffo ametoa maagizo matatu yatakayowanusuru
wanafunzi walemavu wanaosoma katika shule ya msingi ya Makalala Mchanganyiko
iliyopo mjini Mafinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Jaffo ametoa maagizo hayo baada ya juzi
kufanya ziara ya ghafla shuleni hapo ikiwa ni siku kadhaa toka baadhi ya vyombo
mbalimbali vya habari viripoti changamoto zinazowakabiri wakabili wanafunzi na
shule hiyo.
Changamoto hizo ni pamoja na udogo na
uchakavu wa mabweni ya wanafunzi, uhaba wa walimu na watumishi wengine wa shule
hiyo; na ukosefu wa vifaa vya kufundishia na michezo pamoja na mahitaji mengine
mbalimbali muhimu kwa wanafunzi na wafanyakazi wa shule hiyo.
Akiwa shuleni hapo, Jaffo alibaini shule
hiyo kugubikwa na matatizo hayo kwasababu watendaji wa halmashauri ya wilaya ya
Mufindi ambayo awali shule hiyo ilikuwa chini yake na sasa halmashauri ya
Mafinga Mji kwa pamoja wamekuwa hawaifuatilii kwa jicho la jirani pamoja na
kwamba ina mahitaji maalumu.
Waziri huyo alisikitishwa matroni pekee
wa wanafunzi hao wenye ulemavu Faraja Mbilinyi aliposema kwa miaka 15
halmashauri ya wilaya ya Mufindi haijawahi kumlipa malipo yake ya likizo, huku
Mwalimu Agne Jalu mwenye ulemavu wa macho akisema hajawahi kupata malipo kamili
ya likizo tangu aanze kulipwa.
Akitoa agizo la kwanza baada ya
kutembelea mabweni ya shule hiyo na kusikia kilio cha matroni na mwalimu huyo,
Jaffo alisema; “hakikisheni walimu na watumishi wa shule hii ya walemavu na
shule yake dada kama wanadai posho malimbikizo ya posho zao likizo wanalipwa
mara moja na wanapandishwa madaraja haraka iwezekanavyo.”
Akimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi,
Jowika Kasunga kusimamia maagizo aliyokuwa akiyatoa waziri huyo alisema April 1
atapita kwa mara nyingine shuleni hapo ili kujionea utekelezaji wa maagizo yake
ambayo yaliahidiwa na Mkurugenzi wa Mafinga Mji, Shaibu Nnunduma kutekelezwa.
Kuhusu ufinyu wa mabweni na uchakavu
wake, naibu waziri Jaffo alitoa agizo la pili kwa halmashauri ya mji huo ianze
ujennzi wa bweni lingine kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato huku akitaka mpaka mwishoni mwa
mwezi April, magodoro yote katika bweni la wasichana na wavulana wa shule hiyo
yawe yamebadilishwa.
“Mji wa Mafinga ni mji wa biashara,
waiteni wadau wenu, waelezeni matatizo ya shule hii, nina hakika mtachangiwa.
Msissubiri kila kitu kifanywe na serikali kuu, hiyo haitawezekana,” alisema.
Kuhusu vifaa vya kufundishia na
kujifunzia, alitoa agizo la tatu akiitaka halmashauri hiyo kuhakikisha shule
hiyo inakuwa na vifaa hivyo kulingana na mahitaji yake.
Alisema inashangaza kuona watendaji na
wadau wao wengine kila wanapokutana katika vikao vyao wanalipana posho halafu
wakashindwa kupata fedha kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya shule hiyo
maalumu.
Awali Mkuu wa shule hiyo mchanganyiko,
Shem Muheni alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 ina wanafunzi 544 ambao
kati ya 79 ni wanafunzi wenye ulemavu wa akili, ngozi na macho wanaosoma katika
shule maalumu shuleni hapo.
Alisema wakati mahitaji ya walimu katika
shule hiyo ya walemavu ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano, ina mwalimu mmoja
na matroni mmoja aneyalazimika kuwahudumia kwa pamoja wanafunzi wa kike na
kiume.
Alisema uhaba wa vyumba vya kusomea na
mabweni umeifanya shule hiyo ishindwe kupokea idadi kubwa zaidi ya wanafunzi
wanaotaka kujiunga nayo.
Ikiwa katika wilaya inayoongoza kwa kuwa na misitu ya kupandwa nchini(msitu wa Taifa wa Saohill), Muheni alisema wanafunzi hao walemavu wanalala wawili badala ya mmoja kwa kila kitanda huku bwalo la chakula likiwa na meza nne tu wakati mahitaji ni zaidi ya meza kumi.
“Lakini pia hawana nguo, viatu na vifaa vya kujifunzia ambavyo havitoshelezi mahitaji yao ya kila siku,” alisema.
Hivi karibuni Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi alitoa wito kwa wadau wa maendeleo wa wilaya ya Mufindi kujitokeza kusaidia kuzishughulikia changamoto za shule hiyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni