JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi kwa
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, kufuatia vifo vya
wafanyakazi sita wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, vilivyosababishwa
na ajali ya barabarani, iliyotokea leo tarehe 21 Machi, 2016 katika
eneo la Kerege Wilayani humo.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa
tano za asubuhi, baada ya Lori la kubebea mchanga kuyagonga magari
mawili ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambayo yalikuwa katika
Msafara wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na serikali za mitaa,
iliyokuwa akitoka kukagua mradi wa Maji wa Mapinga.
Katika salamu hizo Rais Magufuli
amesema amepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za vifo vya wafanyakazi hao
wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ambao wamepoteza maisha wakiwa
wanatekeleza majukumu ya kikazi.
“Kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa
Pwani naomba kutoa pole nyingi kwa familia za marehemu wote, ndugu,
jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo, naomba Mwenyezi Mungu
awape moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu kutokana na kuondokewa
na wapendwa wao” Amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi. Amina
Aidha, Rais Magufuli amewapa pole wafanyakazi wengine wanane ambao wameumia katika ajali hiyo, na amewaombea wapone haraka.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
21 Machi, 2016
0 maoni:
Chapisha Maoni