ASILIMIA 96 ya wakazi wa mjini
Iringa wakipata huduma ya maji safi na salama, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira Iringa Mjini (IRUWASA) imesema zaidi ya asilimia 30 ya maji wanayosambaza
yanapotea kwasababu mbalimbali ikiwemo wizi.
Mhandisi wa mamlaka hiyo, Jane Malongo
alitaja sababu zingine zinazopoteza maji hayo na hatimaye mapato ya mamlaka
hiyo kuwa ni pamoja na mivujo katika mtandao wake na kuziba kwa mita
zinazotumika kusoma matumizi halali ya maji.
Mhandisi Malango alitoa taarifa hiyo juzi
wakati mamlaka hiyo ikitoa semina kwa wawakilishi wa wanafunzi wa shule za
sekondari za mjini Iringa ya namna shughuli ya uzalishaji maji inayovyofanyika
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maji ambayo kilele chake ni Machi 22.
Katika semina hiyo iliyofanyika katika
moja ya kumbi za mamlaka hiyo, wanafunzi hao walielezwa taratibu za maunganisho
ya maji na walifundishwa jinsi vyanzo vya maji vinavyotunzwa.
Mengine waliyojifunza wanafunzi hao ambao
pia walipata fursa ya kutembelea chanzo cha maji na sehemu ya kutibu majisafi
na majitaka ni pamoja na namna ya kutoa taarifa ya mivujo na ukosekanaji wa
maji, matumizi mazuri ya mtandao wa majitaka na dira na tozo za maji.
Mhandisi Malongo alisema IRUWASA inayokusanya
zaidi ya Sh Milioni 318 kwa mwezi, ina wateja zaidi ya 1,700 wakiwemo wateja 73
wa kibiashara na taasisi 39.
Katika matembezi yao katika chanzo cha
maji na sehemu ya kutibu majisafi na majitaka mtaalamu wa uzalishaji maji wa
mamlaka hiyo, Paulo Mboka aliwaeleza wanafunzi hao hatua zote muhimu
zinazotumiwa na mamlaka hiyo hadi kusambaza maji safi na salama kwa wateja
wake.
Mboka alisema jumla ya mita za ujazo
24,000 za maji zinaweza kuzalishwa na mamlaka hiyo kila siku wakati mahitaji
halisi kwa wakazi wa Iringa Mjini ni wastani wa mita za ujazo 16,000 kwa siku.
Alisema
IRUWASA inaendelea kuusimamia mtandao wa usambazaji majisafi kwa kuhakikisha
inafuatilia na kuziba mivufo yote na kubadilisha mabomba yalichoka wakati
ikiendelea kupanua huduma zake kwenye maeneo ambayo hayana mtandao.
0 maoni:
Chapisha Maoni