Posted byb Esta Malibiche on Dec 9,2016 in NEWS
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Frederick Msigara wa CCBRT katika
hafla ya utoaji tuzo ya mwajiri bora wa mwaka 2015 kwenye ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es salaam.
…………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Mjaliwa
amesema Serikali imetenga sh. bilioni 15 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa
vijana zaidi 2,500 ili kuwajengea uwezo waweze kushiriki kama nguvu kazi
kwenye viwanda vinavyotarajiwa kujengwa nchini.
Alitoa kauli hiyo jana usiku
(Alhamis, Desemba 8, 2016) kwenye sherehe za utoaji wa tuzo ya muajiri
bora wa mwaka 2016, zilizofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Tuzo hizo
zimeandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
Waziri Mkuu alisema Serikali
imeanza kujielekeza katika kutoa mafunzo kwenye sekta za kipaumbele kwa
kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo kama kilimo biashara, mafuta,
gesi, utalii, usafirishaji, ushonaji na bidhaa za ngozi.
Alisema jitihada zinaendelea
kwenye maeneo mengine ili waajiri wawe na wigo mpana wa kuwapata
wafanyakazi wenye stadi stahiki kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa
wao kuwa nguvu kazi yenye ujuzi na umahiri mkubwa kwa lengo la kuongeza
tija.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu alizungumzia changamoto inayolalamikiwa na waajiri ya uwepo wa tozo
mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka tofauti za Serikali kwa huduma
ileile kuwa wanaitambua na tayari mchakato wa kuainisha sheria zote
zinazoonekana kukwamisha uwekezaji pamoja na mazingira ya biashara
nchini.
“Lengo letu ni kuendelea
kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili yaweze kuvutia zaidi
na mchakato huu unashughulikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Tunaomba
mvumilie na mshirikiane nasi katika kuendelea kuziainisha sheria
zinazokwaza biashara ili tuweze kuzijumuisha kwenye mapitio hayo,”
alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
aliwashauri waajiri wote nchini waendelee kufanyakazi zao kwa mujibu wa
sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi. Pia
aliwasihi wafanyakazi wote kufanyakazi kwa bidii na uaminifu mkubwa ili
waajiri waweze kupata faida, hivyo kuwaboreshea maslahi yao
Alisema “tunaposema Hapa Kazi Tu,
tunamaanisha kazi kwenye sekta zote za uzalishaji na utoaji wa huduma
bora nchini, iwe sekta ya binafsi au kwenye utumishi wa umma. Nawasihi
ndugu zangu Watanzania, wekeni nadhiri kwamba katika mwaka 2017 mtafanya
kazi kwa juhudi na maarifa ili kuongeza tija na ufanisi mahala pa
kazi,”.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye
Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama aliwaomba waajiri wawasaidie kuweka
msukumo katika juhudi za kutoa mafunzo kwa ajili ya uzoefu na kuongeza
ujuzi kwa kutoa nafasi kwa wahitimu kupata uzoefu kwenye maeneo yao ya
kazi.
Hata hivyo Mheshimiwa Jenista
alisema anatambua umuhimu wa waajiri na wafanyakazi katika utekelezaji
wa sera ya maendendeleo ya nchi hasa kwa kuongeza ajira kupitia sekta ya
viwanda kwa asilimia 40 kufikia mwaka 2020, mafanikio ya mpango huo
yanategemea mchango wa waajiri kutoka sekta binafsi.
Pia aliwapongeza ATE kwa kutambua
umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu hasa kwa kutoa tuzo katika
eneo la kuendeleza vipaji, ambapo aliwaomba tuzo ijayo waongeze kigezo
cha kumpata mwajiri aliyetumia rasilimali zake kuongeza ujuzi kwa
wafanyakazi wake ambao ndio chanzo cha kuinua tija na ushindani
kibiashara.
“Natambua kuwa ATE mnatoa mafunzo
katika sheria za kazi na usimamizi wa rasilimali watu ambayo husaidia
kupunguza migogoro mahali pa kazi na hivyo kujenga mazingira tulivu
maeneo ya kazi. Naomba kutumia wasaa huu kuwakumbusha waajiri
kuwawezesha wafanyakazi kwenda kuhudhuria mafunzo mbalimbali ili kuweza
kukidhi ushindani katika mazingira ya biashara,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATE,
Dk. Aggrey Mlimuka alisema lengo la uaandaji wa tuzo hiyo ni kutambua
wanachama wenye sera nzuri za usimamizi wa rasilimali watu katika
taasisi na makampuni mbalimbali mwanachama hapa nchini.
Alisema kuwa tuzo hizo zinafuata
mbinu za Kisayansi na kitaalamu ili kuangalia umuhimu wa Rasilimali watu
katika makampuni ya Kibiashara makubwa na madogo na yale ya kati ili
kuinua ujuzi wa wafanyakazi wanaofanya kazi kwa kujituma sehemu za kazi.
Dk. Mlimuka alisema kuwa tuzo hio
pia ilijikita zaidi katika kuangalia maeneo muhimu ya rasilimali watu,
uongozi, utawala, usimamizi wa Rasilimali watu, kusaidia jamii pamoja na
kuwajibika katika jamii, ubora na uzalishaji.
0 maoni:
Chapisha Maoni