Ijumaa, 9 Desemba 2016

MIAKA 55 YA UHURU TANZANIA YAJIVUNIA KUKUA KWA DEMOKRASIA

Posted by Esta Malibiche on Dec 9,2016 in NEWS

umoja
Jovina Bujulu – MAELEZO
Desemba 9, mwaka huu Tanzania itatimiza miaka 55 ya Uhuru ambao ulipatikana mwaka 1961, chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere.
 
Maadhimisho ya Uhuru kwa mwaka huu yanashuhudia kukua na kupanuka kwa wigo wa vyama vya siasa nhini.
Vyama vya siasa ni nguzo muhimu katika ujenzi wa demokrasia na ujio wake umeongeza elimu na maarifa ya siasa kwa wananchi, ambapo wanashiriki kwa kiwango kikubwa katika siasa katika ngazi zote.
Ushuhuda wa kukua kwa demokrasia unajidhirisha katika ushiriki wa vyama vya siasa katika chaguzi mbali mbali kuanzia ngazi za chini hadi juu.
 
Historia inaonyesha kwamba Tanganyika (Tanzania kwa sasa) ilifanya uchaguzi wake wa kwanza mwaka 1962, ambapo kulikua na vyama viwili vya siasa ambavyo ni TANU kilichokua kinaongozwa na Mwalimu Nyerere na chama cha African National Congress (ANC) kilichokua kinaongozwa na Zuberi Mtemvu.
 
Baada ya uchaguzi huo wa mwaka 1962 Tanganyika ikawa taifa la chama kimoja cha siasa (TANU). Wakati huo utaratibu wa uchaguzi uliokuwapo ni kamati Tendaji ya TANU kuchagua watu wawili na kuwapeleka kwa wapiga kura ili kumpata Mbunge na nafasi ya urais ilihusika jina moja lililokuwa linachaguliwa na mkutano mkuu wa TANU na ASP.
 
Mfumo huo ulitumika katika chama tawala yaani chama kimoja ambapo uchaguzi ulifanyika mwaka 1965,1970,1975 mpaka 1990.
 
Mwaka 1992, Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 na mwaka 1995 uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo huo wa vyama vingi ulifanyika ikawa ni miaka thelathini na tatu tangu uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama viwili ulipofanyika mwaka 1962.
 
Mfumo wa vyama vingi vya siasa ni hali ya kuwa na chama zaidi ya kimoja katika nchi moja. Madhumuni ya mfumo huo ni katika nchi yoyote ni kuleta ushindani wa kisiasa ili kuleta maendeleo ya nchi na kuongeza wigo wa demokrasia katika nchi husika.
 
Akizungumzia chimbuko la mfumo huu  nchini, Ndugu John Tendwa ambaye aliwahi kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini alisema kuwa “Kulikuwa na vugu vugu la wanajamii la kuleta msukumo katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, ambao uliungwa mkono na mabadiliko ya kiulimwengu ya kisiasa hasa kuanguka kwa dola za kisoshalisti(dola ya Ulaya Mashariki). Anguka hilo kulifanya jumuiya za Ulaya Mashariki kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi na baadaye kusambaa duniani kote”.
 
Nchini Tanzania uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi vya siasa ulianza kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume ya kuratibu maoni ya watanzania juu ya mfumo gani wa siasa utafatwa nchini. Tume hiyo iliyoongozwa na Marehemu Jaji Nyalali ilikusanya na kuratibu maoni ya wananchi katika sehemu mbali mbali.
 
Tume hiyo ilipokamilisha kazi hiyo, ripoti ilionyesha maoni ya watanzania wachache asilimia 20 ndio waliokubali mageuzi ya vyama vingi na asilimia 80 walipendelea Tanzania ibaki na mfumo wa chama kimoja.
 
Serikali ilianza kufuata maoni ya wachache ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi. Hatua hiyo  ilikua ni uamuzi wa busara kwani ndani ya mfumo huu kuna ushindani wa fikra, mawazo na hatimaye sera na taratibu mbadala za kuongoza nchi kwa misingi madhubuti ya kidemokrasia yenye kuheshimu utu na kulinda haki za binadamu.
 
Hali hiyo huleta msukumo katika harakati za kimaendeleo, ustawi wa maisha na kuzidisha umoja wa haki kwa watu.
Aidha mfumo huo wa vyama vingi nchini ulionekana kama chuo cha siasa za kiukombozi na upanuzi wa wigo wa demokrasia. Jambo hili linajidhihirisha katika chaguzi mbali mbali ambapo wananchi wanapata nafasi ya kuchagua viongozi wa kutoka vyama tofauti vya siasa , kuanzia madiwani, wajumbe na wabunge.
 
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, Tanzania kuna vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu 19, na chama kimoja kina usajili wa muda.
 
Baadhi ya vyama hivyo ni chama cha Mapinduzi (CCM), chama cha Wananhi (CUF), chama cha demokrasia (CHADEMA), Tanzania Labour Party (TLP), NCCR-Mageuzi, ACT Wazalendo na TADEA.
 
Vyama hivi vya siasa vinafanya kazi chini ya Msajili wa vyama vya siasa ambaye ni mwenye dhamana ya kuvisajili na kufuta ambavyo vinakiuka kanuni za maadili ya vyama hivyo za mwaka 1992.
 
Akizungumzia majukumu ya Ofisi yake Msajili wa vyama hivyo Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi alisema kuwa ni pamoja na kugawa ruzuku ya serikali kwa vyama hivyo, kufatilia mapato na matumizi ya vyama hivyo na kusimamia utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010.
 
Vyama vya siasa pia vina haki na wajibu unaoviongoza katika shughuli zake za kisiasa. Haki hizo ni pamoja na kutoa elimu ya uraia na elimu ya uchaguzi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, kutoa maoni ya kisiasa, kujadili na kushindanisha sera za vyama vyao na kushiriki uchaguzi unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
 
Aidha vyama hivyo vina wajibu wa kujieleza kwa wanachama wake ili kuongeza uadilifu wa kisiasa ndani na nje ya chama na kulaani na kuepuka vitendo vya vurugu.
 
Nao baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusu uwepo wa vyama vingi nchini, waliipongeza serikali kwa kuruhusu mfumo huo na kusema kwamba kwa sasa wananchi wengi wanafahamu siasa za nchi pia uwepo wa uwakilishi wa wabunge kutoka vyama mbali mbali bungeni kunaleta changamoto za uwajibikaji zaidi na kuleta maendeleo kwa wananchi waliowachagua.

0 maoni:

Chapisha Maoni