Posted by Esta Malibiche on Dec2,2016 in NEWS
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WATU wanaoishi na
maambukizi ya virusi vya ukimwi wameaswa kuacha kujinyanyapaa ama kukata
tamaa na badala yake wahakikishe wanajilinda na kuepuka maambukizi
mapya ya ukimwi.
Aidha wametakiwa kutumia madawa ya kufubaza makali ya virusi vya ukimwi ARVs kiuhakika.
Rai hiyo imetolewa na
mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, huko Mdaula, wakati wa
maadhimisho ya siku ya ukimwi dunia katika kituo cha kupima na kutoa
elimu juu ya masuala ya ugonjwa wa ukimwi.
Alisema kuwa watu wengi wanaopima na kujikuta na maambukizi hukata tamaa na wengine kuamua hata kujidhuru.
Ridhiwani aliwapa moyo wasijinyanyapae bali wafuate maelekezo ya wataalumu ili kukinga maambukizi mapya.
Hata hivyo alisema pia
ni wajibu wa jamii kuwaheshimu,kuwapa ushirikiano na kuwasaidia
inapobidi ili nao wajione ni sehemu muhimu katika jamii.
Ridhiwani alitoa wito
kwa wananchi jimboni humo kupiga vita maambukizi mapya ya ukimwi kwa
kujilinda na kuwa waaminifu katika mahusiano yao .
“Jukumu la kujilinda ni la watu wote, tuachane na matamanio ambayo mwisho wake ni majuto “” alisema Ridhiwani.
Mbunge huyo alitumia maadhimisho hayo kuungana na wananchi wa Mdaula na baadhi ya wananchi jimbo la Chalinze kupima afya yake.
Katika maadhimisho hayo
watu 81 walijitokeza kupima afya zao ambapo watu watatu kati yao
waligundulika kuwa wana maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
Ridhiwani alianza ziara
yake jimboni hapo yenye lengo la kusikiliza kero za wananchi na kutolea
majibu baadhi ya hatua ambazo zinachukuliwa katika baadhi ya kero ambapo
alianza na kupima afya yake kwenye maadhimisho hayo.
0 maoni:
Chapisha Maoni