Posted by Esta Malibiche on Dec 5,2016 in NEWS
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 17
kati ya vijiji viwili vya Ortukai na Esilalei na Taasisi ya Tanzania
Land Conservation Trust (TLCT) baada ya kukabidhi hati ya shamba la
Manyara Ranch kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli,
Stephen Ulaya.
Hati hiyo imetolewa jana jioni
(Jumapili, Desemba 4, 2016) na Waziri Mkuu katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye kata ya Mto wa Mbu kwenye viwanja vya Barafu baada ya
kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi wa vijiji
hivyo vilivyopo kwenye Kata ya Elesilalei Wilayani Monduli Mkoani
Arusha.
Hatua hiyo imekuja baada ya kilio
cha muda mrefu cha wananchi hao kudai kuwa Rais wa Awamu ya tatu,
Benjamin Mkapa aliagiza shamba hilo ligaiwe kwa wananchi hao lakini
jambo hilo halikufanyika na badala yake watu wachache walijimilikisha
shamba hilo kinyemela chini ya wenyekiti wa bodi ya TLCT.
Waziri Mkuu alisema Serikali
imeamua kurudisha umiliki wa shamba hilo kwa wananchi wa vijiji hivyo
viwili baada ya Baraza la Madiwani na Uongoziwa Wilaya hiyo ya Monduli
kuridhia kwa pamoja umiliki huo kurudi kwa wananchi kama ilivyoamriwa
hapo awali.
“Shamba hili lenye ukubwa wa
ekari 44,930 sasa si mali tena ya Taasisi ya Tanzania Land Conservation
Trust (TLCT) iliyokuwa inafadhiliwa na Shirika la African Wildlife
Foundation (AWF) sasa ni mali ya wananchi na halmashauri ya wilaya ya
Monduli ndio itapanga matumizi bora ya ardhi ya shamba hili mliloteseka
nalo kwa muda mrefu ,” alisema.
Alisema nyaraka zinazoonyesha
kuwa shamba hilo lililotolewa kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na
Ortukai na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu mwaka 1999 kwa ajili ya kilimo
na ufugaji lakini jambo hilo halikufanyika badala yake taasisi ya TLCT
ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.
Hata hivyo Waziri Mkuu alisema
Serikali inaendelea kufuatilia maeneo yote yaliyochukuliwa na watu bila
ya kuyaendeleza na kuwapa wananchi. “Ni kwa nini watu wenye fedha
wanachukua mashamba mkubwa bila ya kuyaendeleza huku wananchi wakiteseka
kwa kukosa maeneo ya kilimo na ufugaji,” alisema.
Awali kabla ya kuhutubia mkutano
huo wa hadhara Waziri Mkuu alitembelea shule ya msingi ya Laiboni
iliyoanzishwa na mzee maarufu wa kimila wilaya huko Laigwanani Meshuko
Ole Mapii ambayo inawanafunzi 102 wakiwemo wajukuu na watoto wa mzee
ambapo alitangaza umiliki wa shamba hilo kurudi kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa William Ole Nasha alisema wizaraya
yake itaendelea kutekeleza Sera za Kilimo nchini pamoja na kusimamia
matumizi bora ya ardhi kwenye shamba hilo kutokana na ukosefu mkubwa
ardhi kwa ajili ya wafugaji na wakulima.
“Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri
Mkuu kuwa tutaendelea kuhakikisha wananchi wafanya ufugaji wa kisasa
wenye kwa tija kwa kutumia shamba hili. Pia nakupongeza Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo na
maagizo uliyotupa ya kuhakikisha wananchi wanatumia ardhi hiyo vizuri
tutayasimamia,” alisema.
Baada ya shamba hilo kurudishwa
kwa wananchi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema
‘’Nashukuru leo umiliki wa shamba hili umebadilishwa na naishukuru
Serikali yangu tulivu kwa kutoa hati hii kwa Mkurugenzi wa wilaya ya
Monduli ili wananchi waweze kunufaika na ardhi yao na sio watu wachache
wanaolipwa mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi’’.
Naye Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mheshimiwa Jumanne Maghembe aliwasihi wananchi hao kuheshimu
njia za mapito ya wanyama (ushoroba) katika eneo hilo ambalo wanyamapori
kutoka hifadhi za Tarangire, Manyara na Ngorongoro wanalitumia kwa
ajili ya kupita kwenye hifadhi hizo mara kwa mara.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
amempa siku mbili Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mazingira wa wilaya ya
Monduli , Adil Mwanga kumuondoa muwekezaji, Lekisongo Meijo katika
shamba lenye ukubwa wa ekari 2,800 lililoko katika kijiji cha Lemoti
tarafa ya Kisongo ambalo alimilikishwa bila ya kufuata taratibu na
kulirudisha kwa wananchi.
Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Bw. Gambo kufanya uchunguzi wa umiliki wa mashamba mengine
makubwa ambayo yana migogoro na hayajaendelezwa mkoani humo likiwemo la
Makuyuni Stein Seed Valley na kuipatia ufumbuzi migogoro hiyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni