Ijumaa, 30 Desemba 2016

MHANDISI MAKANI ATOA WIKI MBILI KWA WAFANYAKAZI NGORONGORO KUWASILISHA TAARIFA ZA MIFUGO NA MAJENGO YA KUDUMU WANAYOMILIKI NDANI YA HIFADHI HIYO

Posted by Esta Malibiche on Dec 30,2016 in NEWS

aga
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati)
akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wilayani
Ngorongoro mkoani Arusha jana katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji
wa maagizo ya Waziri Mkuu. Kulia
ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Freddy Manongi na Mbunge wa Jimbo la
Ngorongoro ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha(kushoto)
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia)
akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wilayani
Ngorongoro mkoani Arusha jana katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa
maagizo ya Waziri Mkuu,  ametoa wiki mbili kwa watumishi wenye mifugo na
majengo ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi hiyo kujiandikisha kwa uongozi wa
mamlaka hiyo ikiwa ni mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu.
 

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole
Nasha akichangia katika mkutano huo. Alieleza kuwa salama ya Hifadhi ya
Ngorongoro itategemea uwekaji wa mizania sawa baina ya uhifadhi na maendeleo ya
wananchi wa eneo hilo.
 Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,
Freddy Manongi (katikati) akizungmza katika mkutano huo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani na 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof.
Alexandre Songorwa (kulia).
 Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Mfaume Taka (kushoto) akizungumza kwenye
mkutano huo.
 Sehemu ya watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
wakiwa kwenye mkutano huo.
……………………………………………………………………………………
NA HAMZA TEMBA – WMU
…………………………………………….
 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhandisi Ramo Makani ametoa wiki mbili na siku tano kwa watumishi wote wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wenye mifugo na majengo ya kudumu
ndani ya eneo la hifadhi hiyo kuorodhesha majina yao kwa uongozi wa mamlaka
hiyo  na kusalimisha taarifa ya kile wanachokimiliki ndani ya eneo hilo
ikiwa ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji maagizo ya Waziri Mkuu
aliyoyatoa kwa uongozi wa mamlaka hiyo.
 
Ametoa agizo hilo jana wakati
akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama
ya wilaya na Ngorongoro katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa makao
makuu ya NCAA yaliyopo katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa ajili ya
kufuatilia changamoto za uhifadhi na utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa aliyoyatoa kwa mamlaka hiyo hivi karibuni akiwa ziarani mkoani
Arusha.
 
Anasema miongoni mwa maagizo
yaliyotolewa na Waziri Mkuu ambayo yameshaanza kufanyiwa kazi ni pamoja na
kuondolewa mifugo yote maeneo ya Kreta, kuhakikisha upatikanaji wa maji na
chumvi kwa ajili ya mifugo na wananchi, idadi ya mifugo kutambuliwa na kupigwa
chapa pamoja na kutambua idadi ya wananchi ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi
ya Ngorongoro na kupewa hati za utambuzi.
 
“Mpaka ikifika wiki ya pili ya mwezi
januari, tarehe 15, kila mtumishi ambaye yeye binafsi ana mifugo ndani ya eneo
hili, maana tunaanzia nyumbani, Conservator (Mhifadhi) uweke utaratibu wa
kupokea taarifa kutoka kwao, kila mmoja aweze kudeclare (kutangaza) umiliki
wake wa mifugo ndani ya eneo la hifadhi, ng’ombe, mbuzi, kondoo.
 
“Lakini pia kila mtumishi ambaye
ana nyumba ya kudumu ndani ya hifadhi, iliyojengwa kwa matofali, mabati, zege
nakadhalika atuambie, na mimi nishauri tu kuwa muwazi itakusaidia. Kwasababu
haiwezekani sisi tuanze kuwaambia watu wengine, wewe kwanini umejenga nyumba ya
kudumu hapa, wakati tunapowaonyesha vidole na wengine sisi tunazo, hatuwezi
kwenda kuwaambia wengine, wewe kwanini una mifugo humu 200,000, 2000, 1000 au
500 wakati wengine sisi humu tuna mifugo zaidi yao hata mara mbili”,
alisisitiza Makani.
 
Alisema kuwa, kwa wale waajiriwa
wapya wapewe elimu juu ya malengo na majukumu mahsusi ya taasisi hiyo pamoja na
miiko yake ambayo ni pamoja na uwepo wa maeneo maalum ya uhifadhi
yasiyoruhusiwa mifugo na majengo ya kudumu.
 
Amewataka watumishi wa mamlaka hiyo
kusoma kwa makini madhumuni ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo pamoja na majukumu
makhsusi iliyopewa ili kufanya vizuri zaidi katika uhifadhi endelevu wa Hifadhi
hiyo huku wakitambua kuwa wao ndio wenye jukumu la kwanza la kuhakikisha kuwa
taasisi hiyo inastawi.
 
Katika hatua nyingine Naibu Waziri
Makani ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa NCAA kumkabidhi taarifa ya
mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu. “Zile wiki mbili
nilizozisema, ule mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya waziri mkuu, sina
maana kwamba tutaanza kutekeleza kwenye wiki mbili, hivi tunavyoendelea
kutekeleza kwa maana yapo mambo mengine hapa utekelezaji wake ni wa muda zaidi
ya hizo wiki mbili, nataka nipate mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo hayo
tuujadili na kuufanyia kazi kwa haraka”.
 
Alisema miongoni mwa changamoto kubwa
za uhifadhi katika eneo hilo kwa sasa ni wingi wa mifugo pamoja na majengo ya
kudumu ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro jambo lililohatarisha
uhifadhi endelevu wa hifadhi hiyo.
 
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa
Mamlaka hiyo, Dkt. Freddy Manongi amesema jukumu kuu la kuazishwa kwa mamlaka
hiyo ni kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori na malikale, utalii na jamii iliyopo
ndani ya Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
 
Akizungumzia changamoto  alisema
kuna uhaba wa chakula kutokana na wananchi wa eneo hilo kuzuiliwa kulima
kisheria, malalamiko kuhusu wanyama wakali kuwashambulia wananchi na ongezeko
la magonjwa mbalimbali huku mengi yakisababishwa na muingiliano wa wananchi
na  wanyamapori.

0 maoni:

Chapisha Maoni