Posted by Esta Malibiche on Dec 30,2016 in MICHEZO
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, imeiadabisha Tanzania Prisons kwa bao 1-0 katika
mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa
Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho
kwa Azam FC mwaka huu kabla ya kuukaribisha mwaka mpya ‘2017’, bao hilo
pekee limewekwa kimiani na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, dakika ya 40
baada ya kupokea pasi safi ya Joseph Mahundi na kuwahadaa mabeki wa
Prisons kisha kupiga shuti la kiufundi lililojaa kimiani.
Azam FC iliingia kwenye mchezo huo
ikiwa na sura mpya kwenye benchi la ufundi lililosimamiwa na makocha wa
timu yake ya vijana, Idd Nassor Cheche na Idd Abubakar na hii ni
kufuatia kuwasitishia mikabata wakufunzi kutoka Hispania wakiongozwa na
Kocha Mkuu, Zeben Hernandez.
Hiyo inamaanisha kuwa makocha hao
wa muda wameanza kibarua chao vema kwa kujiandikia rekodi ya kuiongoza
Azam FC kushinda mchezo wa ligi katika mechi yao ya kwanza wakiwa
benchini.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii
waliuanza mchezo huo vema wakifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa
Prisons, lakini safu yao ya ulinzi ilikuwa imara kuondoa hatari zote
wakiongozwa na Salum Kimenya.
Alikuwa ni Bocco aliyeihakikishia Azam FC bao la uongozi hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika.
Kipindi cha pili Azam FC iliongeza
nguvu kwa kuwaingiza Shaaban Idd, Himid Mao na Samuel Afful, lakini
jitihada za kusaka mabao zaidi zilishindikana kutokana na uimara wa safu
ya ulinzi ya Prisons.
Kiungo Frank Domayo, alikaribia
kuipatia bao la pili Azam FC dakika ya 50 akiwa anatazamana na kipa wa
Prisons, lakini shuti aliloopiga lilitoka pembeni kidogo ya lango la
wapinzani wao.
Dakika moja baadaye mshambuliaji
wa Azam FC, Yahaya Mohammed, alifanya jitihada binafsi za kuwatoka
mabeki wa Prisons lakini shuti alilopiga lilitoka nje ya lango la
Prisons.
Prisons ilipata pigo dakika ya 69
baada ya kiungo wao mkabaji, Kazungu Mashauri, kuonyeshwa kadi nyekundu
kufuatia kumfanyia madhambi ya makusudi winga wa Azam FC, Mahundi ambaye
alishindwa kuendelea na mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na
nahodha msaidizi, Himid Mao.
Hadi dakika 90 zimalizika ubao wa
matokeo ulikuwa ukisomeka vilevile na hivyo kufanya Azam FC kuondoka na
pointi zote tatu zinazoifanya kufikisha jumla ya pointi 30 katika nafasi
ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi 14 na kinara Simba (44)
na 10 kwa upande wa Yanga waliojikusanyia 40.
Huo ni ushindi wa kwanza wa Azam
FC kwenye mechi za mzunguko wa pili wa ligi baada ya kuanza vibaya kwa
kutoka sare mechi mbili mfululizo dhidi ya African Lyon (0-0) na
Majimaji (1-1).
Azam FC kwa sasa inaelekea kwenye
changamoto nyingine ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo
itaanza kufungua dimba Jumatatu ijayo kwa kucheza na Zimamoto saa 10.15
jioni ndani ya Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.
Kikosi cha Azam:Aishi Manula,
Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan
Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo, Yahaya Mohammed/Shaaban dk 64,
John Bocco/Samuel Afful dk 90, Joseph Mahundi/Himid dk 71
0 maoni:
Chapisha Maoni