Jumatatu, 12 Desemba 2016

KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM CHAFANYA TATHMINI YA UCHAGUZI MKUU WA 2015, MAAZIMIO KUPELEKWA NEC JUMANNE

Posted by Esta Malibiche on Dec12,2016 in SIASA

Na Bashir Nkoromo, Dar
Kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichofanyika leo chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, kimefanya tathimni ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana, na kuibuka na mambo kadhaa ambayo yatafikishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa CCM (NEC) keshokutwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jioni hii, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye amesema, tathmini hiyo ya uchaguzi, imefanywa na Kamati Kuu ikiwa ni sehemuya utamaduni wa CCM, kufanya thathmini kila baada ya uchaguzi mkuu.

"Tathmini hizi hutusaidia sana, kujua wapi tulifanya vizuri na wapi hatukufanya vizuri na mengineyo yote yaliyokuwa sehemu ya ushiriki wa Chama katika uchaguzi mkuu, na tumekuwa tukifanya hivi katika chaguzi zote hali ambayo imeifanya CCM kuimarika zaidi", alisema Nape.

Alisema, mapendekezo au hoja zote zilizoibuliwa na wajumbe katika kikao hicho cha Kamati Kuu ya CCM zitawasilishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM-NEC, ambacho kitafanyika keshokutwa, jijini Dar es Salaam.

Nape amesema, pia kwamba, kutokana na kufanyika vizuri na kwa umahiri mkubwa, Kikao cha Kamati Kuu kimemalizika leo, na hakitakuwepo kesho kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam

0 maoni:

Chapisha Maoni