Jumatatu, 12 Desemba 2016

HALMASHAURI YA CHALINZE YAJIPANGA KUDHIBITI WAKWEPA USHURU

Posted by Esta Malibiche on Dec 12,2016 in NEWS

23
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu, akizungumzia mikakati waliyojiwekea kuinua mapato .
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
………
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
HALMASHAURI ya Chalinze, wilayani Bagamoyo,inatarajia kununua mashine za EFD ,kumi zitakazogharimu sh.mil.16 kwa lengo la kuinua mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya wizi.
Mashine hizo sio za kwanza kununuliwa katika halmashauri hiyo bali zinaongezwa ili kusambazwa kwenye maeneo ambayo yanakata ushuru bila kutumia risiti kwasasa.
Akizungumzia mikakati waliyojiwekea kuongeza mapato hayo,mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Saidi Zikatimu,alisema wamegundua kuna maeneo ambayo makusanyo yanashuka kutokana na kukosa mashine hizo.
Alisema wanakusudia kuinua mapato katika vyanzo vya mapato ya ndani kwa kusimamia kikamilifu vizuia vyote vinavyokesha kukusanya mapato.
Alielezea kuwa mbali ya hilo wameanza kudhibiti njia zote za panya hasa maeneo ya vijijini .
Zikatimu alisema wameweka kizuia cha Lugoba kinachokusanya mapato ya kokoto,kizuia cha Chalinze,Kiwangwa,Msata na Vigwaza ambavyo vyote vinakesha.
‘Tunataka pia kuweka kizuia kingine pale Msoga ambapo tumesikia kuna magari mengine yanapenya katika maeneo hayo hayafiki Chalinze.Kizuia kingine kinawekwa Kihangaiko ili kudhibiti magari yanayokwepa kupita Tanga”alisema Zikatimu.
Aidha alisema wanaongeza wakusanyaji na wasimamizi kizuizi cha Saadan ambako wamegundua mkaa mwingi unatoroshwa na kupelekwa Zanzibar hivyo wanapambana ili usivushwe .
Zikatimu anafafanua,changamoto kubwa ni halmashauri hiyo kuwa kubwa na kugawanyika hivyo wakwepa kodi na ushuru kutumia kigezo hicho hivyo kutokana na hilo wameongeza nguvu eneo la Gongo na Miono.
Alisema kuna watendaji ambao bado wanaonekana kufanya ubabaishaji na wezi wa mapato ambapo wanawachukulia hatua za kisheria na wengine kesi zao zipo mahakamani.
Hata hivyo alieleza,mapato yanaenda vizuri kwani wamejiwekea bil 3.65 katika mapato ya ndani licha ya kuwa bado hawajapokea fedha yoyote ya miradi ya maendeleo kutoka serikali kuu hadi sasa .
Nae diwani wa kata ya Lugoba,Rehema Mwene,alihoji juu ya kuwekwa bajeti ya mil1.6 kwa kila mashine hizo wakati zipo za gharama ya chini kuanzia laki 6 hadi 7.
Alisema mapato ya halmashauri hiyo yamekuwa yakipanda na kushuka hivyo njia ya kudhibiti hali hiyo ni kuongeza mashine hizo.
“Ni vyema zingeongezwa hadi kufikia mashine 50 kwa wakati mmoja kwani itatusaidia kuwa na uhakika wa mapato lakini mtindo wa kunutia vitabu vya risiti ni wa zamani lazima tubadilike,” alisema Rehema.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze,Isaac Kama alisema watanunua mashine 10 na kuziweka kwenye maeneo wanayotumia vitabu vya risiti ikiwa ni pamoja na magulio,minada,zahanati kwenye fedha za CHF na vituo vya afya.
Alibainisha kwamba zipo aina tatu za mashine hizo na bei tofauti na wamechagua ya kati yenye ghama ya mil 1.6 huku wakiwa ameshauriwa na mkoa wachukue hiyo kwani inadumu kipindi kirefu .

0 maoni:

Chapisha Maoni