Jumatatu, 9 Oktoba 2017

KIGWANGALLA ATANGAZA VITA DHIDIYA MAJANGILI

Posted by Esta Malibiche On Oct 9,2017IN NEWS

K1
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Andrea Kigwangala akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi.
K2
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Daniel Shonza akizungumza na waandishio wa habari mara baada ya hafla ya kuapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
K3
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Said Jafo akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi.
Picha na: Frank Shija – MAELEZO
……….
Jonas Kamaleki-MAELEZO
Muda mfupi baada ya kula kiapo, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, ametoa onya kali kwa majingili nchini na kuwataka kuacha mara moja vitendo hivyo.
Dkt. Kigwangalla ametoa onyo hilo leo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuapishwa mawaziri na naibu mawaziri.
“Majangili waanze kukimbia wenyewe pale wanapowaona wanyama kwani tutawashughulikia ipasavyo na kuhakikisha tunakomesha vitendo hivi viovu katika nchi yetu,” alisema Dkt. Kigwangalla.
Kuhusu utalii, Dkt. Kigwangalla amesema kuwa watalii wamekuwa wakiongezeka lakini si kwa kiwango cha kuridhisha hivyo Serikali itafanya juhudi za makusudi kutangaza vivutio vya utalii kwa njia za kisasa ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa ubunifu katika kujitangaza itabidi utumike ili kuhakikisha Tanzania inavutia watalii wengi kutoka nje hususan soko jipya la China na nchi nyingine ikiwemo Marekani na nchi za Ulaya.
Kwa kufanya hivyo pato la Taifa kutokana na utalii litaongezeka kuliko ilivyo sasa, alisema Kigwangalla.
Aidha, Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amesema atashirikiana na wizara nyingine kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji ili lipatikane suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo, amesema atahakikisha watumishi wa umma katika wizara yake wanafanya kazi kwa kujituma zaidi na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.
Kwa mujibu wa Jafo, uadilifu, uwajibika na nidhamu ni mambo ambayo yatatiliwa mkazo katika wizara yake ili kuwa na utumishi wenye tija.
Amewataka wakuu wa mikoa, wilaya kufanya kazi kwa mashindano ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo katika sehemu husika na kuchochea ukuaji wa uchumi hasa wa viwanda.
“Wakuu wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri muwe vinara katika utendaji wenu mkiwasimamia walioko chini yenu kwa weledi ili muweze kwenda na spidi ya Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Jafo.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akizungumza baada ya kuapishwa amesema atahakikisha sekta ya habari inapewa kipaumbele kwani habari ni jambo muhimu katika suala zima la mawasiliano.
Mhe. Shinza atahakikisha weledi katika sekata ya habari unazidi kuimarishwa ilikuondoa upotoshwaji ambao umekuwa ukijitokeza katika baadhi ya vyombo habari.
Kuhusu upatikanaji wa habari kwa sehemu kubwa ya watanzania, Shonza amesema atajitahidi kufanya habari ziwafakie watanzania wengi Zaidi ili kujenga jamii yenye ufahamu wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi yao.
Katika hafla hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha jumla ya Mawaziri nane na Manaibu Mawaziri 16 ambao wameanza kazi mara baada ya kuapishwa kwa kuhudhuria kikao cha Maalum cha Baraza la Mawaziri.
Baadhi ya mawaziri waliokula kiapo leo ni Mhe. Angella Kairuki (Madini), Mhe. George Mkuchika (Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe. Hamis Kigwangwalla (Maliasili na Utalii) na Suleiman Jafo (Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).
Kwa upande wa Manaibu Mawaziri, Mhe. Rais amewaapisha jumla 16 ambao baadhi yao ni Mhe. Stella Manyanya (Naibu waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Mhe. William Ole Nasha (Elimu, Sayansi na Teknolojia), Dkt. Faustine Ndungulile (Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), Mhe. Stella Ikupa (Ofisi ya Waziri Mkuu, Watu wenye Ulemeva) na Mhe. Juliana Shonza (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo)

0 maoni:

Chapisha Maoni