Posted by Esta Malibiche on Oct 25,2017 IN MICHEZO
Judith Ferdinand, Mwanza
Zaidi ya shilingi Milioni 40 za kitanzania zinatarajiwa
kushindaniwa katika mashindano ya mbio za Rock City Marathon 2017,
zinazotimua vumbi Oktoba 29 mwaka huu katika viunga mbalimbali vya Jiji
la Mwanza na kutamatikia katika uwanja wa CCM Kirumba.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na washiriki wa ndani na
nje ya nchini ikiwemo kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan ya Kusini,
Marekani na China.
Kutakuwa na makundi matano, kundi la kwanza ni umbali wa km
42, la pili km 21, la tatu km tano, la nne km tatu huku la tano likiwa
la mita 100, 200, 400, 800 na 1500.
Hayo yalisemwa na Bidan Lugoe ambaye ni mratibu wa
mashindano hayo yanayoandaliwa na kampuni ya Capital Plus
International, yakilenga kuendeleza mchezo wa riadha pamoja na
kuutangaza utalii.
Alisema mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya nane
mfululizo awali yalikua yakifanyika kwa km 21 “half marathon”, ingwa
kwa mwaka huu yameboreshwa zaidi na yatakuwa na urefu wa km 42 “full
marathon”.
Jumla ya milioni 40 zitatolewa kama zawadi katika
mashindano haya, ambapo mshindi wa kike na kiume kila mmoja atapatiwa
zawadi ambapo wa kwanza kwa mbio za km 42 atapata milioni nne, wa pili
milioni mbili, wa tatu milioni moja na km 21 wa kwanza atajinyakulia
milioni mbli, wa pili milioni moja na watatu laki tano.
Kwa upande wa km tano ambapo watashiriki watu wenye
ualibino, mshindi wa kwanza atajinyakulia kitita cha shilingi 150,000,
wa pili 100,000 na wa tatu 50,000 ikiwa ni njia ya kupinga mauaji ya
watu hao, ambapo pia kutakua na zawadi kwa mbio za ndani ya uwanja za
mita 100, 200, 400, 800 na 1,500 kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari ikiwa ni kukuza mchezo wa riadha.
Lugoe Alisema hadi sasa zaidi ya washiriki 500 wa ndani ya
nchini na 70 kutoka nje nchini wameisha jisajili na kwamba usajili bado
unaendelea hivyo matarajio ni kuwa na washiriki kati ya 4000 na 5,000
katika mbio hizo.
Mbio hizo zitaanza majira ya saa 12 asubuhi hadi 12 jioni
siku ya jumamosi Oktoba 29 yakianzia na kutamatikia uwanja wa CCM
Kirumba ambapo pia itakuwa ni fursa kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na
viunga vyake kukutana ili kujionea mbio hizo ikiwa ni sehemu ya burudani
pia.
0 maoni:
Chapisha Maoni