Jumatatu, 23 Oktoba 2017

Waziri wa Maliasili Dk.Kigwangalla afanya mkutano wa kihistoria na wadau Dodoma

Posted by Esta Malibiche on Oct 23,2017 IN NEWS
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangall,akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya Maliasili na utalii mkoani Dodoma

Mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta ya maliasili na utalii ukiendelea Mkoani Dododma.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla mapema leo Oktoba 22,2017 amefanya mkutano wa kwanza  na wa kihistoria kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya Maliasili na Utalii katika mkutano wa kupokea maoni na kusikiliza hoja za msingi ili kusaidia maendeleo ya Wizara hiyo.
Katika mkutano huo zaidi ya Wadau 150 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini walipata kutoa maoni  na mapendekezo yao kwa Waziri Dkt. Kigwangalla namna ya kusaidia maendeleo ya sekta ya Maliasili na Utalii hapa nchini.
Baadhi ya maoni na hoja zilizoibuka kutoka kwa wadau hao ni pamoja na kutaka kuruhusiwa kusafirisha viumbe hai kama vipepeo, vyura na vingine ambayo vinapatikana kwenye hifadhi na Maliasili za Taifa,
Pia wadau hao waliomba kuruhusiwa suala la usafirishaji wa magogo nje ya nchi huku suala la sera ya kusimamia biashara ya mkaa ili kudhibiti uchomaji wa misitu na maliasili hapa nchini.
Kwa upande wa Wapagazi walitaka mikataba yao pamoja na kuongeza malipo mazuri kwani wao ni miongoni mwa wadau muhimu katika suala la ukuaji wa Uchumi kupitia Utalii hapa nchini.
Hata wadau hao waliomba Waziri awe makini katika Wizara yake hiyo kwani miongoni mwa Wizara ngumu na zenye kuondosha Mawaziri wanaopitia Wizara hiyo  mara kwa mara.
Kwa upande wake Waziri Dkt. Kigwangalla akifafanua  baadhi ya mambo aliweza kuwatoa wasiwasi wadau hao kuwa yeye ameaminiwa na Mh. Rais na atasimamia maadili.
“Mimi sihongeki, sinunuliki na wala sishawishiki kwa rushwa bora nife kwa heshima zangu kuliko kuaibika kwa kutotenda haki.” Alieleza Dkt. Kigwangalla.
Na kuongeza: "Ukija kwangu njoo na ‘issue’ ambayo iko ‘straight’ imefuata taratibu za kisheria yenye maslahi mapana kwa Taifa" alisema Dkt.Kigwangalla.
Hata hivyo, Dkt.Kigwangalla amebainisha kuwa kwa sasa lengo kuu ndani ya Wizara hiyo ni kufikiria tofauti.
"Tufikilie ubunifu zaidi kuongeza vivutio vyetu kwa sasa Kaskazini inakalibia kuhelemewa,tupo mbioni kuwa na vivutio zaidi hasa ukanda wa Kusini. Tunaamini ukalimu kwa watalii wetu ni kitu muhimu sana. Wenzetu wanasema njoo kwetu utauona mlima, basi sisi tuseme njoo kwetu utaupanda mlima kilimanjaro, tuongeze ubunifu" alieleza Dkt. Kigwangalla akiwataka wadau na wakuu wa taasisi za Wizara hiyo.
Hata hivyo Waziri Dkt.Kigwangalla aliwatoa wasiwasi wadau hao ni kuwaeleza kuwa, baada ya kikao hicho cha Dodoma, anatarajia kutembelea kila sekta na kufanya majadiliano kwa undani.
Aidha, akihitimisha mkutano huo na wadau, Dkt. Kigwangalla amesema kuwa pamoja na kuwekewa lengo la kufikisha watalii Milioni 2, ifikapo mwaka 2020, amewahakikishia wadau hao kuwa watahakikisha wanavuka lengo mahususi ya idadi hiyo kwani wamejipanga kuendesha Wizara hiyo kwa kisasa zaidi.
Mwisho.

0 maoni:

Chapisha Maoni