Posted by Esta Malibiche on Oct 9,2017 In NEWS
MKUU wa wilaya ya Kinondoni Ally Hapi (alievaa suti nyeusi) akikata utepe wakati akizundua taasisi ya BUTA- Vicoba Endelevu yenye maskani yake Bunju wilayani humo jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Rais wa Vicoba Endelevu nchini Bi Devotha Likokola (alieshika kipaza sauti) na Mkurugenzi wa Taasisi ya BUTA- Vicoba Endelevu Bi Semeni Gama (kulia kwa DC Hapi).
MKUU wa wilaya ya Kinondoni Ally Hapi ameuomba uongozi wa Vicoba Endelevu hapa nchini kuhakikisha wanatanua mtandao wao uweze kuwafikia wananchi wengi zaidi wakiwemo walimu, wafanyakazi wengine wa serikali pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo ili kuisaidia serikali kufanikisha adhma yake ya kuyakomboa makundi hayo kiuchumi.
Hapi alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati akizundua taasisi ya BUTA- Vicoba Endelevu iliyopo Bunju wilayani humo.
“Niwaombe sana viongozi wa Vicoba mtanue zaidi mtandao wenu ili muwafikie maelfu zaidi ya wafanyabiashara ndogo ndogo, wafanyakazi mbalimbali wa serikali wakiwemo walimu na mshirikiane nao katika kuangalia namna bora zaidi ya wao kupata huduma za kifedha ikiwemo mikopo ili waongeze thamani ya mitaji yao,’’ alisisitiza.
Zaidi, alitoa wito kwa wakina baba wahakikishe wanahamasisha wake zao pamoja na mabinti zao waweze kushiriki katika Vicoba ili kuinua vipato vya familia zao.
“Mbali na wakina mama pia hebu tuwahamasishe zaidi wasichana ambao wamekuwa wakitumia muda na pesa zao katika urembo na kujipodoa na badala yake sasa wajenge utamaduni kujijenga kiuchumi zaidi kwa kushiriki katika vikundi hivi vya kijasiliamali pamoja na Vicoba,’’ alisema.
Awali akitoa taarifa ya hali Vicoba endelevu hapa nchini, Rais wa Vicoba Endelevu nchini Bi Devotha Likokola alisema mtandao huo tayari unahusisha vikundi zaidi ya laki moja vikiwa na wanachama zaidi ya milioni mbili na laki mbili huku wakiwa na akiba ya zaidi ya Tsh Trilioni moja na milioni mia mbili.
“Nitoe wito tu kwa wanajamii wazidi kushiriki katika Vicoba endelevu kwa kuwa ni mfumo ambao tayari umeonyesha kuwa unaweza kuwaonda katika umaskini,’’ aliomba.
Akiizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya BUTA- Vicoba Endelevu Bi Semeni Gama alisema taasisi hiyo inahusisha vikundi 128 kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya, Kigoma, Lindi, Tanga na Njombe ikiwa ina jumla ya wanachama hai 2,186 huku ikiwa na mtaji wa zaidi ya sh milioni 560.
Pamoja na mafanikio hayo, Bi Semeni alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa eneo ambalo lingetumiwa na taasisi hiyo kuanzisha mradi mkubwa wa kufuga kuku na kuanzisha shule ya chekechea.
Hata hivyo, katika hotuba yake DC Hapi aliahidi kumuagiza Mkurugenzi wa Manispaaa hiyo kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo kwa kuipatia ardhi taasisi hiyo kupitia mradi wa upimaji ardhi unaoendelea katika maeneo ya Mapwepande na Wazo.
Mbali na wanachama kutoka vikundi mbalimbali vya Vicoba, shughuli hiyo pia ilihusisha uwepo wa taasisi mbambali za kifedha zikiwemo benki za ACB, CRDB, Benki ya Posta pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF
MKUU wa wilaya ya Kinondoni Bw Ally Hapi (alievaa suti nyeusi) akikagua baadhi ya bidhaa zinazoandaliwa na wajasiliamali ambao ni wananchama wa Vicoba Endelevu baada ya kizundua taasisi ya BUTA- Vicoba Endelevu yenye maskani yake Bunju wilayani humo jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
MKUU wa wilaya ya Kinondoni Bw Ally Hapi (alievaa suti nyeusi) akiongoza maandamano ya wajasiliamali ambao ni wananchama wa Vicoba Endelevu kuelekea kwenye ofisi za taasisi ya BUTA- Vicoba Endelevu yenye maskani yake Bunju wilayani humo jijini Dar es Salaam ambapo alizindua ofisi hizo mwishoni mwa wiki.
0 maoni:
Chapisha Maoni