Posted by Esta Malibiche on JUNE 19,2017 IN MICHEZO
Frank Shija – MAELEZO
SERIKALI imesema kuwa hakuna
chombo chochote cha habari kitakachochukuliwa hatua kwa kuandika habari
zenye mrengo wa kukosa sera na utekelezaji wake kama ambavyo wadau wengi
wamekuwa wakiaminisha umma.
Kauli hiyo imetolewa leo na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbasi wakati
akizungumza katika Kipindi cha Habari Kuu kinachorushwa na Kituo cha
Televisheni cha Startv mjini Dodoma.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Sheria na
12 ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51 kinatoa ruhusa kwa
chombo cha habari kukosoa kwa lengo la kuonyesha njia mbadala katika
kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“Hakuna chombo cha habari
kitakachochukuliwa hatua kwa kukosoa, haki hiyo ipo kwa mujibu wa Sheria
ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51, tutaendelea kuthamini
na kufanyia kazi ukosoaji huo,” alisema Dkt. Abbasi.
Hata hivyo Dkt. Abbasi amesisitiza
kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa chombo kitakachokiuka sheria
na misingi ya maadili ya taaluma ya habari kwa lengo la kulinda maslahi
ya taifa.
Dkt. Amesisitiza kuwa ni vyema
wamiliki wa vyombo vya habari wakatumia uhuru huo wa kisheria kuchapisha
habari zenye nia njema kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi badala ya
kueneza hofu miongoni ya mwa jamii.
Akijibu swali la muongozaji wa
Kipindi kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la Mawio, Dkt. Abbasi amesema kuwa
Gazeti hilo halijafungiwa kutokana na kuandika habari ya kukosoa
Serikali isipokuwa limekiuka miiko ya taaluma kwa kuandika habari za
kushushia heshima na hadhi ya mtu katika jamii pamoja na kukiuka maagizo
halali ya Serikali.
Alisema kuwa kama ingekuwa
kulifungia Gazeti hilo kwa sababu ya kuandika habari za kukosoa pengine
lingekuwa limefungiwa muda mrefu kutokana na ukweli kwamba Gazeti hilo
mrengo wake unafahamika kuwa ni wa ukosoaji.
Akizungumzia dhana ya uhuru wa
habari, Dkt. Abbasi amesema kuwa ipo haja ya wadau wa habari kufahamu
dhana halisi ya uhuru wa habari badala ya kuendelea kufanya makosa ya
tafsiri isiyo sahihi jambo ambalo linapotosha dhana nzima ya uhuru wa
habari.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Mkataba
wa Kimataifa wa mwaka 1966 wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ibara ya 19
inaeleza haki za kupata habari ambayo inaenda sambamba na ukomo wa kutoa
taarifa kwa maslahi ya nchi.
Aidha Dkt. Abbasi ametoa rai kwa
wadau wa habari nchini kuisoma sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016
iliyoanza kutumika rasmi badala ya kuyaachia makundi ya wanaharakati
wapotoshe uhalisia wake.
Akizungumzia utekelezaji wa Sheria
hiyo, Dkt. Abbasi amesema kuwa sheria imekwishaanza kutekelezwa katika
hatua kadha ambapo alizitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na
utoaji wa Vitambulisho vya Waandishi wa HabarI.
Alisema kuwa utoaji wa
Vitambulisho hivyo umelenga kuwajengea uwezo wa kujiendeleza waandishi
wa habari katika kipindi cha mpito cha miaka mitano ili kufikia vigezo
stahiki vya taaluma.
Tanzania imeingia katika Historia
baada ya kutunga Sheria na 12 ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 ambayo
imefuta Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ambayo imepitwa na wakati
kutokana na mabadiliko ya teknolojia, uchumi na utamaduni
0 maoni:
Chapisha Maoni