Alhamisi, 15 Juni 2017

MADIWANI WAGOMA MAFUNZO WAKITAKA POSHO YA SH 100,000

Posted by Esta Malibiche on JUNE 15,2017 IN NEWS


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamegoma kupewa mafunzo ya utaratibu ulioboreshwa wa uendeshaji wa Miradi ya Maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGDG), wakishinikiza kupewa posho ya Sh 100,000 kwa siku.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), yalitakiwa kufanyika jana katika ofisi za Halmashauri hiyo na kuwahusisha madiwani pamoja na wakuu wa idara.
Hata hivyo madiwani wote waligoma na kutoka nje, jambo lililosababisha wakufunzi kutoka Tamisemi kutoa mafunzo hayo kwa wakuu wa idara peke yao. Kabla mafunzo kuanza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Michael Kilawila aliwaeleza madiwani hao kuwa, kwa sababu mafunzo hayo hayapo kisheria, halmashauri inatakiwa kutoa posho zao kutoka makusanyo ya ndani.
Alisema, kutokana na mapato ya halmashauri kuwa madogo, kila diwani atalipwa Sh 60,000 kama posho ya siku, hivyo kwa siku mbili za mafunzo hayo kila diwani angelipwa Sh 120,000.
Baada ya tamko hilo madiwani walionesha kutoridhishwa na kiwango hicho cha posho na kuanza kugonga meza wakishinikiza kulipwa Sh 100,000 kwa siku kama wanavyolipwa katika vikao vingine vinavyotambulika.
Kilawila aliwasihi madiwani hao wakubali posho hiyo, lakini waliendelea kugoma, na kuamua kutoka nje, wakiwaacha wakuu wa idara ndani ya ukumbi.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Butamo Ndalahwa alisema, madiwani hao wamegoma kwa sababu ya kutaka posho kubwa bila kujali kuwa mafunzo hayo yangewanufaisha wananchi ambao ndio waliwachagua.
Alisema mafunzo hayo yanatolewa katika halmashauri zote nchini kwa lengo la kuhakikisha madiwani wanashirikiana na wananchi kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo halmashauri itawasaidia kuiendeleza.
Ndalahwa alisema, kitendo cha madiwani kugomea mafunzo hayo kitasababisha maendeleo ya halmashauri hiyo kurudi nyuma kwa sababu ya kukosa elimu ya uibuaji wa miradi ambayo inakubalika.
Alisema amesikitika sana kuona madiwani wanaweka maslahi mbele badala ya kuwatumikia wananchi ambao waliwachagua “tumewaelimisha sana sababu ya kuwapa posho ya Sh 60,000 lakini hawakutaka kuelewa badala yake walianza kugonga meza ovyo na kutoka nje.”

0 maoni:

Chapisha Maoni